Mafia ni kisiwa kinachovutia kwa utalii kwani inavyo vivutio vingi:
Vivutio vilivyopo ndani ya Wilaya ni pamoja na (Uasilia na magofu ya kale)
MAGOFU
a. Uasilia wetu wa Mafia Tabia, chakula, makazi na Vazi letu (cultural tourism) huu unapatikana maeneo yote ya kisiwa kikuu na visiwa vidogo vinavyoizunguka Mafia
kama, Juani, Jibondo, Chole na Bwejuu. Pia chakula asilia na mapishi ya pekee ya mboga ya pwani na samaki wa kupaka.
b. Miji iliyozama katika eneo la kijiji cha Mlongo.
c. Magofu ya soko la watumwa ambayo yako katika kisiwa cha chole.
d. Magofu ya Mfalme Njozi katika kijiji cha Kanga.
e. Makaburi ya shekhe na sharifu ambayo yapo katika kijiji cha Kungwi na ndani ya msitu wa Ngome – Mlola.
HIFADHI YA MSITU WA MLOLA.
Msitu wa mlola ni moja kati ya misitu ya ukanda wa pwani ambao una mandhari nzuri na aina mbalimbali ya viumbe hai ikiwemo miti ya aina ya pekee. Kima wa blue (blue monkey), chesi, ndolo, mijusi ya aina ya pekee (yellow & blue lizard). Baadhi ya miti maarufu katika msitu huu ni pamoja na; mibuyu, mikulukalemba, mikwaju mwitu, mizambarau, milola na midimu mwitu.
Vivutio vingine vilivyopo ndani ya msitu huu wa Mlola (ngome) ni pamoja na visima vya kalingwa msitu wa jadi majogoloni na msitu wa kijiji cha Bweni ambao uko pembezoni mwa msitu wa Mlola – Bilingiti. Msitu huu una umaarufu wa pekee ikiwa ni kuwa na visima asilia na ambavyo ni dawa (kisima upele).
Kivutio kikubwa na ambacho kimeufanya msitu huu kupata umaarufu kwa jina lake ni mwamba mkubwa wa mawe ya matumbawe yaliyokufa (dead coral). Mwamba huu ndio unaokinga kisiwa kutokana na pepo kali za kusi na kaskazi upande wa mashariki mwa kisiwa na mawimbi makubwa ya bahari kuu. Mara nyingi watafiti hufika katika maeneo haya na kuona mpangilio wa miamba na namna ilivyozaliwa.
MISITU YA MIKOKO (MANGROVE FOREST)
Hii ni misitu ya ukanda wa pwani ambayo huanzia mwisho wa maji kutoka (low tide) na mwisho wa maji kujaa (High tide) Misitu hii imekuwa maarufu sana kwa kua ni moja ya kiashiria kikubwa cha mabadiliko ya hali ya hewa. Na tafiti nyingi za mabadiliko katika dunia ambayo husababishwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira hufanyika kwenye misitu ya mikoko. (good indicator for climatic change.) Pia misitu hii imekua kivutio kikubwa cha utalii na sehemu kubwa ya mapumziko ya wageni.
VIUMBE WA BAHARINI POTWE (WHALESHARK)AU PAPA USINGIZI.
Papa usingizi; hawa ni viumbe wakubwa wa baharini ambao ni wapole na rafiki wa binadamu. Hawa wamekuwa kivutio kikubwa na ambacho kinaingizia wilaya yetu pato na ajira kwa wajasiriamali wadogo wadogo, sehemu kubwa ya pato linatokana na viumbe hawa limekuwa likipotea kutokana na kutosimamia ipasavyo.
ARDHI OEVU(WETLANDS)
Maeneo haya yamekuwa na umuhimu wake hasa kwa kuzingatia kuwa yana viumbe wake na wanyama kama viboko ambapo ni maajabu makubwa viboko kupatikana katika maeneo ya kisiwa kinachozungukwa na bahari. Kazi kubwa iliyopo ni;
kuyatambua mabwawa yote yaliyopo hapa wilayani.
kuyaandalia mipango ya usimamizi kwa ushirikiano na wadau mbalimbali – kamati za vijiji na serikali za vijiji.
Kuwatenga viboko kwenye mabwawa Machache kama bwawa la urungwi kijiji cha Gonge, Utumaini kijiji cha Gonge, Nyamvura kijiji cha kilongwe na bwawa la mwamizi kijiji cha Ndagoni ambayo yatasimamiwa na kuendelezwa kwa ajili ya utalii.
MISITU YA JADI ILIYOPO MAFIA.
Mafia imekuwa na misitu midogo na yenye miti ya asili ambayo haipatikani mahali pengine popote Tanzania. Hii ni kutokana na msimamizi wa asili na utamaduni wa kuhifadhi mazingira kwa njia asilia. Misitu asilia ya jadi iliyopo na inayotambuliwa ni Majogoloni, Duzini, Mlongo, Tarrain, Kijiwe nyara, Msitu wa Hifadhi kijiji cha Juani, Visiwa vya shungimbili na mbarakuni. Wilaya kupitia mpango huu wa uboreshaji wa utalii na hifadhi ya mazingira itavitangaza vivutio hivi kwenye tovuti ya wilaya baada ya kuboresha na kuondoa mapungufu madogo madogo yaliyopo, kama
kutengeneza njia za miguu, rail guide/walk way kutengeneza na kuweka vibao.
UJENZI WA GATI
Mafia ni kisiwa ambapo wakazi wake hutumia usafiri wa maji (Bahari) na anga (Ndege) Wakazi waliowengi hutumia usafiri wa Bahari kutokana na gharama kubwa ya usafiri wa anga. Hata hivyo usafiri wa maji si salama kutokana na vyombo vinavyotumika utokuwa na bima pamoja na usalama wa vyombo vyenyewe ( Boti na Jahazi). Hata hivyo kwa sasa ujenzi wa Gati umekamilika licha kuwepo kwa changamoto kwa upande wa pili yaani Nyamisati hutokuwa na gati. Kujengwa kwa Gati sehemu ya Nyamisati kutasaidia sana wakazi wa Mafia pamoja na Wafanyabiashara kuingia na kutoka kisiwani. Kwa sasa bado wananchi hutumia Boti na Jahazi za mbao kusafiri kutoka Mafia hadi Nyamisati.
MNARA WA KUONGOZA MELI (1893)
Mnara uliotengenezwa mwaka 1893 na Serikali ya Kikolini ya Kijerumani kwa ajili ya kulinda usalama wa bahari na nyumba iliyotengenezwa 1843 kwa ajili ya mtumishi wa mnara huu ambapo sasa pamekua mahali pa mapumziko ya kitalii. Mnara huu umekuwa ni kivutio cha watalii hasa kwa kuzingatia kuwa uko ndani ya Msitu wa Mlola na mwishoni mwa kisiwa cha Mafia, ( Kaskazini). Mnara huu pamoja na kuwa unasimamiwa na Bandari, jukumu la kuutangaza na kuutumia liko chini ya Halmashauri ya wilaya
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.