Ili kuhakikisha elimu inaboreshwa nchini, Serikali iliweka jitihada ya kujenga vyuo vya VETA 25 vya wilaya ili kuwawezesha vijana kuwa na uwezo wa kutumia maarifa wanayopata kujiajiri pamoja na kuongeza ufanisi kwa wale wanaopata ajira rasmi sehemu mbalimbali.
Miongoni mwa wilaya zilizonufaika na hatua hiyo ni wilaya ya Mafia ambapo matunda yameanza kuonekana baada ya chuo cha VETA wilayani hapo kutoa wahitimu 51 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 2024.


Akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya chuo hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo amewataka wazazi kulipa kipaumbele suala la elimu kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu katika ngazi tofauti kwa kuwapeleka shule pamoja na vyuo ili kuwajengea msingi mzuri katika maisha yao.
Mhe. Mangosongo amewasisitiza wazazi kuwaandikisha vijana chuoni hapo mara tu nafasi za masomo zinapotangazwa maana Serikali imejizatiti kutoa elimu bora kwa kuboresha miundombinu pamoja na kuweka samani na vifaa ili vijana wapate ujuzi utakaowasaidia kuchangia maendeleo ya Taifa.


Aidha, amewasisitiza wanafunzi wanaoendelea na masomo chuoni hapo kutodanganyika na vishawishi vyovyote na badala yake wazingatie masomo na lengo lililowapeleka chuoni ili waongeze ujuzi utakaosaidia kuwakomboa kiuchumi na kuchangia maendeleo nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Mafia Ndugu Salim Jumbe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuinua sekta ya elimu nchini kwa kuanzisha vyuo vya VETA ili kuwasaidia vijana, pia ametoa wito kwa vijana kujiunga na kozi zinazotolewa chuoni hapo za muda mrefu na muda mfupi maana Serikali imeweka gharama nafuu kuhakikisha wananchi wengi wananufaika.


Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.