Wanawake wilayani Mafia wametakiwa kushirikiana kupitia jukwaa la uwezeshwaji wanawake kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo ambazo hutolewa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili waweze kupiga hatua katika shughuli za kujipatia kipato.
Wito huo umetolewa leo Julai 10, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo wakati akizungumza na wajumbe wa Jukwaa la Uwezeshwaji Wanawake Kiuchumi katika hafla ya ufunguzi wa jukwaa hilo kiwilaya.
Mhe. Mangosongo ameeleza kuwa kwa kudumisha upendo, umoja na mshikamano wanawake wanaweza kupiga hatua kubwa kiuchumi wakiinuana katika fursa mbalimbali ikiwemo za ujasiriamali na kushiriki majukwaa mbalimbali ambayo yanaweza kutangaza kazi zao.
Pamoja na mambo mengine, amewataka wanawake kutumia jukwaa hilo kusambaza elimu baina yao pamoja na jamii nzima dhidi ya ukatili wa kijinsia ambao umekuwa ukikithiri hasa kwa watoto, ambapo amewataka kuimarisha malezi kwa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo viovu.
Aidha, amewataka kuendelea kudumisha amani hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu huku wakiwa mabalozi kwa kueleza mazuri yanayofanywa na Serikali.
" Mwaka huu 2025 ni mwaka wa uchaguzi, tutumie nafasi hii kuwaelimisha wananchi kufuata njia sahihi ya kujitokeza kupiga kura pamoja na kuendelea kudumisha amani yetu" alisisitiza Mhe. Mangosongo.
Wajumbe wa jukwaa hilo walipata fursa ya kuchagua viongozi katika nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Katibu Msaidizi pamoja na wawakilishi wawili katika ngazi ya mkoa ambao wataongoza kwa miaka mitatu hadi Juni 2028.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.