Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imeadhimisha kilele cha wiki ya chanjo kiwilaya leo Aprili 30, 2025 kwa kutoa elimu kwa kina mama na wasichana.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mhe. Aziza Mangosongo amewataka wazazi kuwa makini kwa kuwapeleka watoto katika vituo vya kutolea huduma ya afya kupata chanjo ili kuzuia magonjwa ya mlipuko kama Polio na Surua Rubella.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kushirikiana katika malezi ya watoto hasa kwa kina baba kuhudhuria kliniki na wenza wao bila kuwaachia majukumu hayo wanawake peke yao.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa zoezi la uchanjaji, Mratibu wa Chanjo wa Wilaya Ndugu Hussein Rajab ameeleza kuwa Wilaya inatarajia kufika asilimia 96 ya kiwango cha uchanjaji kutoka asilimia 90, hatua ambayo inachangiwa na uanzishwaji wa huduma ya chanjo katika zahanati mpya ya Kibada iliyopo kata ya Baleni.
Ndugu Rajab ameeleza kuwa baadhi ya changamoto zilizopo ni pamoja na baadhi ya wanajamii kuwa na imani potofu kuhusu chanjo zitolewazo kwa watoto, na kuwataka wazazi kuachana na imani hizo ili wajitokeze kupata elimu ya chanjo na kukamilisha dozi kama inavyotakiwa.
Baadhi ya wazazi waliowapeleka watoto wao kupata chanjo wametoa wito kwa wazazi wenzao kuzingatia umuhimu wa chanjo kwa watoto wao kama inavyoshauriwa." Nawahamasisha kina mama wenzangu kuwaleta watoto kupata chanjo na kufuata ushauri na maelekezo ya daktari kwa kuzingatia umuhimu wa chanjo hizo" alisema Khadija Issa, mkazi wa kata ya Kilindoni.
Vituo 26 kati ya vituo 28 vilivyopo wilayani Mafia vinatoa huduma ya chanjo vituoni na kupitia huduma za mkoba katika ngazi ya jamii.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya chanjo inasema kwamba " Chanjo ni Kinga, Tuungane Kuwezesha Walengwa Wote Wapate Chanjo".
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.