Mkuu wa Wilayaya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo ametoa onyo kwa wananchi wanaojihusisha na vitendo vya ukatili kufuatia vitendo vya uvunjifu wa sheria dhidi ya watoto ikiwemo ajira za utotoni pamoja na unyanyasaji.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika leo Juni 16, 2025, Mhe. Mangosongo amewataka wananchi kuzingatia sheria zinazomlinda mtoto dhidi ya unyanyasaji wowote pamoja na kuwanyima watoto haki za msingi ikiwemo elimu kwa kutoa ajira za utotoni.
" Kwa upande wa Mafia, ajira nyingi za utotoni tunazipata kwa wavuvi, na hiyo ni kinyume cha sheria na taratibu na ni kumkosesha mtoto haki ya kusoma na kutimiza ndoto zake. Niwatake wamiliki wa mitumbwi, mabaharia na manahodha kutowachukua watoto kwenda nao kwenye uvuvi" alisema Mhe. Mangosongo akisisitiza kuwa Serikali haitoruhusu vitendo hivyo vishamiri bila kuchukua hatua stahiki.
Mhe. Mangosongo ameeleza kuwa vitendo vya unyanyasaji kwa watoto ni jambo ambalo hatolifumbia macho kwa kuhakikisha kuwa wahalifu wanachukuliwa hatua ili kukomesha ukatili kwa watoto hasa ikizingatiwa kuwa vitendo vya ukatili wilayani Mafia bado vimeendelea kukithiri kwa muda mrefu.
Kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, jumla ya matukio 463 ya ukatili yaliripotiwa katika dawati la polisi na ustawi wa jamii wilayani ambapo matukio yanayoongoza kuripotiwa ni ukatili wa kijinsia kwa kuwa na matukio 245, ukatili wa kimwili matukio 111, ukatili wa kutelekezwa matukio 63 pamoja na ukatili wa kingono matukio 54 yakiwemo matukio ya mimba za utotoni.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi kushirikiana na walimu na viongozi mbalimbali katika jamii kutokomeza tabia ya utoro kwa wanafunzi ambapo matukio mengi ya kihalifu hufanywa na wanafunzi watoro kwa kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria kama utumiaji wa dawa za kulevya, na kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo, jambo ambalo hupelekea mimba za utotoni.
Kuanzia Januari mwaka huu 2025 hadi sasa, mimba za utotoni tisa (9) zimeripotiwa wilayani Mafia, hivyo wananchi wameendelea kupewa wito kuripoti vitendo vya ukatili katika jamii kwani Serikali imeanzisha dawati la jinsia na watoto ili kurahisisha utoaji wa huduma na kunusuru watoto dhidi ya vitendo viovu ambapo vituo vya kipolisi 420 kote nchini vinatoa huduma kwa wananchi.
Kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka huu 2025 ni " Haki za Watoto, Tulipotoka, Tulipo na Tuendako".
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.