Wakazi wa Mafia waaswa kuunga mkono jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi na salama.
Hayo yamebainika leo Aprili 28, 2025 wakati wa warsha ya wadau mbalimbali iliyohusu matumizi ya majiko banifu kama suluhisho la Nishati Safi ya Kupikia.
"Kinachofanyika leo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi na salama katika kutunza mazingira" alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Ndugu Mussa Kitungi, alipokuwa akifungua warsha hiyo.
Lengo la mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Mutina Power Afrika, ni kuendeleza juhudi za utunzaji mazingira kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha na kufanya mabadiliko katika matumizi ya nishati.
" Mradi wetu unakuja kubadilisha mtazamo wa wananchi katika nishati ya kupikia kutoka kutumia kuni na mkaa na kutumia mkaa mbadala" alisema Afisa Mradi kutoka Mutina Power Afrika, Bi. Jackline Mtemahanji.
Ameongeza kuwa wataendelea kuomba ushirikiano wa Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha wanaungana kuboresha mazingira kwa kutumia nishati safi.
" Hapo mwanzo nilikuwa nikitumia sana kuni na mkaa, ila baada ya kushiriki mafunzo kuhusu matumizi ya jiko la nishati safi, nitakuwa wa kwanza kuhamasisha wenzangu kutumia nishati safi hasa kwa wachakataji wa samaki, mama lishe wenzangu na wengine" alisema Bi. Aisha Salum, mjasiriamali kutoka kata ya Kilindoni.
Hapo awali, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Juma Salum alitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa hiyo ili kutumia teknolojia mpya ya nishati ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni ambayo yamekuwa si rafiki kwa mazingira.
Majiko hayo yanayotumia mkaa utokanao na mabaki ya vifuu vya nazi, machicha na makumbi ya nazi na mabaki mbalimbali ya mazao ya shambani, yanatarajiwa kuuzwa kwa bei ya punguzo kutoka Shilingi 125,000 hadi kufikia Shilingi 35,000 kwa wakazi wa Mafia, na baadhi ya majiko yatatolewa bure kama mfano
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.