Elimu bora ni haki ya msingi kwa kila mwanafunzi, bila kujali hali aliyonayo.
Abdul Hassan Ulongo (15) mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Kilindoni wilayani Mafia, alishindwa kufika shuleni kwa miezi sita kutokana na kushindwa kutembea kwenda shuleni kwa sababu ya hali yake ya ulemavu aliyokuwa nayo.
" Nimeshindwa kufika shule tangu mwezi wa pili mwaka huu kwa sababu nimekuwa nikishindwa kutembea na ninaishi mbali na shule" alisema Abdul, mwanafunzi mwenye ulemavu.
Kwa kutambua changamoto yake, ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri kupitia Idara ya Elimu ilifanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na uongozi wa shule kumpatia Kitimwendo (Wheelchair) pamoja na mahitaji mengine ya shule kama madaftari, Kalamu, sare na chakula awapo shuleni.
" Tunahitaji ushirikiano kutoka kwenu katika kumsaidia Abdul awapo shuleni kwa kumuonesha upendo. Abdul asaidiwe kufika shule na kumrudisha nyumbani baada ya masomo" alisema Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia, Olivanus Thomas aliyemuwakilisha Mkuu wa Wilaya Mhe. Zephania Sumaye, alipokuwa akiongea na wanafunzi wa Sekondari ya Kilindoni.
"Tunafanya utaratibu ili ahamishiwe kwenye shule ya bweni ya watu wenye uhitaji maalum" alieleza ndugu Olivanus.
Mara nyingi wanafunzi wenye matatizo mbalimbali kwenye jamii yetu hushindwa kuhudhuria shuleni kutokana na changamoto mbalimbali, hali inayopelekea walimu na wanafunzi wenzao kuhusisha hali hiyo na utoro.
"Kama Kuna wanafunzi wenye matatizo kama haya mitaani na nyumbani, tuwasemee ili wapate haki zote kama afya na elimu maana ulemavu haumzuii mtu kufikia malengo yake" alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Mwl. Kassim Ndumbo.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.