Wanawake wajasiriamali waliopo kisiwani Chole wilayani Mafia, wanatarajia kupata soko la kimataifa la zao la mwani kwa kutangaza bidhaa zitokanazo na zao hilo amabazo zitaongeza mnyororo wa thamani.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) Bi. Audrey Azoulay aliyepotembelea Wilayani Machi 04, 2025 kwa lengo la kushuhudia shughuli mbalimbali zinazohusu uhifadhi wa mazingira na kuona jinsi ambavyo UNESCO inaweza kusaidia juhudi hizo.
" Tuna furaha kuwa hapa kwa sababu kisiwa cha Mafia ni miongoni mwa maeneo yaliyo katika uhifadhi na tunatarajia kuisaidia jamii katika shughuli zake za kimazingira kwa kufanya kazi na wakulima wa mwani, wavuvi na wadau mbalimbali wanaofanya kazi kutunza mikoko" alieleza Bi. Azoulay. Hivyo tunatambua changamoto zinazoikabili dunia katika uchafuzi wa mazingira" aliongeza.
Akielezea namna walivyovutiwa na shughuli za uongezaji wa thamani wa zao la mwani, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Ali Mwadini amefurahishwa na wanawake wajasiriamali kisiwani Chole na kuahidi kuwapa nafasi wajasiriamali hao kwa kuwapeleka wanawake watatu kwa niaba yao kutangaza bidhaa zao nchini Ufaransa ili kujitengenezea soko.
Wajasiriamali hao wamepongeza Serikali kwa jitihada hizo ambazo zitachangia uchumi endelevu kisiwani Mafia na kitaifa kwa ujumla.
" Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa wageni wetu na Serikali waliofika kusikiliza kero za wajasiriamali na kutambua mafanikio yetu kwa ujumla, tunaamini shughuli zetu zitafanikiwa " alisema Mwabia Rajabu, Mkulima wa mwani kisiwani Chole.
Ukulima wa mwani pamoja shughuli nyingine kama uvuvi, zinafanikiwa kutokana na uhifadhi mzuri wa mazingira ambao unachangiwa na wadau mbalimbali kama Hifadhi ya Bahari Mafia ( HIBAMA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ( NEMC), pamoja na jamii ambao ni wanufaika wakubwa wa mazao ya bahari.
" Tunawekeza na kuwezesha hifadhi hai ya maliasili kama njia mojawapo ya kuhifadhi maliasili ambapo wanajamii wanakuwa ni kipaumbele kusimamia maliasili wanazozitegemea, hivyo ujio wa Mkurugenzi Mkuu wa masuala haya ya bayoanuai ni mkubwa sana kwa nchi yetu na ni heshima kwa Wanamafia hasa katika masuala ya kulinda ikolojia na uchumi wa wanajamii wanaotegemea rasilimali hizi" alieleza Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mkurugenzi Mkuu NEMC.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumualika Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO nchini Tanzania kwakuwa ujio wake umekuwa wa mafanikio na unaendeleza kuifungua Mafia katika Utalii, kuitangaza katika uchumi kwa kuwawezesha wajasiriamali kupata masoko , pamoja na kuendeleza shughuli za uvuvi endelevu ambavyo vyote kwa ujumla vitaipatia mapato Halmashauri.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.