Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imetakiwa kuongeza nguvu katika usimamizi wa mapato na kuendelea kutenga fedha za kukamilisha miradi iliyosimama kwa muda mrefu.
Akitoa maagizo hayo Juni 19, 2025 kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani lililolenga kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG), Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Pwani Sehemu ya Mipango na Uratibu Bi. Edna Katalaiya, ameeleza kuwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato utasaidia kuongeza pato la Halmashauri ambalo litatumika katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili wananchi wapate huduma iliyokusudiwa.
" Tunaelekezwa kwenye miongozo ya uandaaji wa bajeti za Serikali kwamba, kabla hatujaanza miradi mipya, tuhakikishe miradi viporo imekamilika na itoe huduma kwa wananchi" alisisitiza Bi. Katalaiya.
Pamoja na mambo mengine, Halmashauri imetakiwa kuhakikisha inabuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kusimamia vyema vyanzo vilivyopo kwa kuongeza wigo wa ukusanyaji na kuanzisha miradi mikakati itakayosaidia kuongeza mapato na kukuza ajira kwa vijana.
Katika hatua nyingine, Bi. Katalaiya amewasisitiza wakuu wa Idara na Vitengo kusimamia matumizi mazuri ya mfumo wa kujibu hoja na kuondokana na matumizi ya karatasi katika kujibu hoja mbalimbali na kuwasisitiza kudumisha umoja katika utendaji kazi na kuhakikisha hawazalishi hoja mpya.
Hadi kufikia Juni 15, 2025 Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imefanikiwa kufunga hoja 16 kati ya hoja 34 za mwaka wa fedha 2023/ 2024.
Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kupata Hati safi kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2020 hadi sasa, pamoja na kukusanya asilimia 96 ya mapato mpaka kufikia tarehe 17 Juni, 2025 hali ambayo inatoa mwelekeo mzuri wa kufikia lengo la kukusanya asilimia 100 na zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Juma Salum ameipongeza Serikali kwa kuleta mabadiliko makubwa ndani ya miaka mitano, hatua ambayo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuchochea uwekezaji katika kisiwa cha Mafia hasa katika utalii , pamoja na kuleta fedha za utekelezaji wa miradi ya elimu, afya, maji, umeme na barabara.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.