Utangulizi.
Wilaya ya Mafia ni Miongoni mwa Wilaya sita (6) katika Mkoa wa Pwani. Wilaya zingine ni pamoja na Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe, Mkuranga na Rufiji. Kijiografia Wilaya ya Mafia ni mkusanyiko wa Visiwa vinane kwenye Bahari ya Hindi km 195 kusini mwa Jiji la Dar es Salaam. Visiwa hivyo ni Mafia (kisiwa kikuu), Jibondo, Mbarakuni, Shungimbili, Nyororo, Juani, Bwejuu na Chole. Visiwa vya Mbarakuni, Shungimbili na Nyororo ni vya makazi ya muda tu ya wavuvi. Kisiwa cha mafia kinapatikana kati ya longitudi 39°E – 40°E na latitude 7.38oS.
ENEO NA MIPAKA YA WILAYA.
Wilaya ya Mafia ina Eneo la kilometa za mraba 972, kati ya hizo Kilometa za mraba 407 ni nchi kavu na 565 ni eneo la maji ya Bahari ya Hindi ambayo ni sawa na asilimia 58.73 ya eneo lote. Upande wa kaskazini, Mafia imepakana na Wilaya za Mkuranga na Kibiti, kusini Magharibi na wilaya ya Kilwa na upande wa kusini Mashariki imepakana na Bahari ya Hindi.
IDADI YA WATU.
Katika Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Wilaya ilikuwa na watu 66,180 wanaume 33,220 na wanawake 32,960 ikiwa na ongezeko la asilimia 3.6 kwa mwaka na wastani wa watu 4 kwa kaya.
HALI YA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI.
Wilaya ya Mafia ina jumla ya viwanda 20 kati ya hivyo, kimoja (1) ni kikubwa, vinne (4) vya kati na kumi na tano (15) vidogo. Viwanda hivi vinajumuisha viwanda vya uchakataji wa mazao ya bahari,viwanda vya mafuta ya nazi,ufyatuaji tofali,utengenezaji wa samani,uzalishaji wa barafu na ushonaji. Aidha, Wilaya ya Mafia kuna hoteli za kitalii nane (8) na nyumba za kulala wageni (Lodging Houses) kumi na nane (18) na nyumba za kulala wageni (Guest Houses) kumi na nne (14). Pia wilaya ya Mafia ina vituo vya kuogelea (Diving Center) tatu (3). Hadi sasa Wilaya ya Mafia ina jumla ya Maduka ya nusu jumla(sub-wholesaler) tisa (9) na rejareja na biashara zinginezo zipatazo mia sita sitini na nane (668). Sambamba na uwepo wa biashara hizi, wilaya ya Mafia tuna uhitaji mkubwa kwenye fursa mbalimbali za uwekezaji katika maeneo tofauti kama ifuatavyo:
FURSA ZA KIUCHUMI ZILIZOPO.
i. Bahari
Kilimo cha Mwani. Miaka ya hivi karibuni, kilimo cha mwani kimekuwa ni shughuli muhimu sana kiuchumi ikisaidia kupunguza kasi ya uvunaji wa samaki na mazao mengine ya bahari. Kwa wilaya ya Mafia, zao la Mwani limekuwa na manufaa kwa kuongeza kipato na ajira kwa kina mama kwa kuwa hawakuwa na fursa ya kujishughulisha na shughuli nyingine zaidi ya uvuvi. Kwa mwaka 2022/23 jumla ya tani 690 za mwani zilivunwa. Fursa nyinginezo katika kilimo cha Mwani ni pamoja na kuchakata na kuongeza thamani ya zao la mwani, kutengeneza bidhaaa mbalimbali zitokanazo na mwani.
Vivutio vya Utalii.
Mazalia ya Samaki matumbawe na Michezo ya Uzamiaji (Diving and Snorkling) Idadi kubwa ya vivutio vilivyopo baharini kunaifanya Mafia kuwa sehemu ya utalii wa kuzamia yenye hadhi ya kidunia (world class diving/snorkeling site). Kisiwa cha Mafia ni eneo muhimu la mazalia ya samaki linalokadiriwa kuwa na zaidi ya aina 400 za samaki. Pamoja na uwepo wa vivutio hivi vya baharini, bado idadi ya watalii wazamiaji imekua ni ndogo. Hivyo, juhudi za makusudi za kukitangaza kisiwa cha Mafia kama kituo cha michezo ya uzamiaji zitasaidia kuleta na kuongeza watalii wa ndani na nje.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.