Watumishi wa afya wilayani Mafia waaswa kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa chanjo ili kuzuia magonjwa.
Wito huo umetolewa Mei 9, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo wakati wa kikao maalum cha kutambulisha chanjo ya pili ya Polio ambapo pamoja na kutilia mkazo suala la chanjo, ametumia fursa hiyo kuhamasisha jamii kujenga vyoo bora na kutunza mazingira ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.
" Afya ni kila kitu katika maisha yetu, kama afya ikitetereka hata maisha yetu ya kila siku hatuwezi kuwa na maendeleo. Polio asilimia kubwa ya kuenea kwake ni uchafu, hivyo tujitahidi kuwa wasafi katika uandaaji wa vyakula, miili yetu, kuhakikisha watoto wanapata chanjo pamoja na kujenga vyoo bora" alisema Mhe. Mangosongo.
Kwa upande wake, Afisa Afya wa Wilaya ya Mafia Ndugu Othman Masanga ameeleza kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea kuenea kwa ugonjwa wa Polio ni pamoja na kinyesi, maji machafu na matapishi, hivyo ameendelea kutoa wito kwa jamii kuzingatia usafi katika shughuli zao za kila siku.
Baadhi ya wajumbe waliohidhuria kikao hicho wameishukuru Idara ya Afya kwa kuwapa elimu na kuahidi kusambaza elimu hiyo katika jamii ili wananchi waweze kuepukana na magonjwa.
" Tumepewa taratibu na kuelekezwa kuanza chanjo, elimu tumepata hivyo tutakwenda vijijini kuelimisha wananchi ili wapate elimu ya kutosha juu ya maana ya chanjo na hasara za kutochanja" alieleza Ndugu Ngweshani Bakiri, Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Wilaya ya Mafia.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.