Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo ametoa wito kwa jamii kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kutokomeza ugonjwa wa malaria kwa kufuata ushauri unaotolewa na wataalam wa afya pamoja na kuzingatia usafi katika mazingira yanayowazunguka.
Wito huo umetolewa leo Juni 17, 2025 wakati wa uzinduzi wa Afua ya Viuadudu ( Biorlavicide) iliyofanyika eneo la Kigamboni lililopo kata ya Kilindoni ambapo Mhe. Mangosongo aliambatana na Idara ya Afya kutembelea eneo hilo kwa lengo la kupulizia dawa katika bwawa ambalo limekuwa chanzo kikubwa cha mazalia ya mbu.
" Nitoe wito kwa wataalam wa afya kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kupambana na malaria, vilevile niwaombe wazazi kuwa makini kwa kuhakikisha watoto hawachezi maeneo haya hatarishi na kuhakikisha wanatumia chandarua kuzuia kuenea kwa malaria pamoja na kwenda vituo vya kutoa huduma ya afya pindi wanapopata changamoto za afya, badala ya kutumia dawa bila kufika vituoni" alieleza Mhe. Mangosongo.
Kwa upande wake, Afisa Afya wa Wilaya ya Mafia Ndugu Othman Masanga ameeleza kuwa Idara ya Afya inaendelea kutoa elimu kuhusu afya, hasa kupambana na malaria kwa jamii kutumia vyandarua na kusafisha mazingira kuzuia mazalia ya mbu ili Wilaya iweze kutimiza lengo la Serikali la kutokomeza kabisa malaria ( Zero Malaria) ifikapo mwaka 2030.
Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imeendelea na afua za kupambana na kukabiliana na ugonjwa wa malaria na kupelekea kupungua kwa maambukizi toka asilimia 22.9 kwa robo ya Oktoba hadi Desemba 2024 mpaka asilimia 18.5 kwa robo ya Januari hadi Machi 2025.
Katika hatua nyingine ya kuhakikisha ugonjwa wa malaria unatokomezwa, Mhe. Mangosongo ameielekeza Wakala ya Barabara Tanzania ( TANROADS) kutengeneza mitaro itakayosaidia kuondosha maji ambayo yamekuwa yakituama katika eneo hilo kwa muda mrefu na kuwa kero kwa wakazi wanaozunguka bwawa hilo.
" Niwape pole wakazi wanaozunguka eneo hili lakini niwahakikishie kwamba Serikali yetu chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali na itaendelea kuchukua hatua nzuri kutatua kero zenu. Naielekeza TANROADS kuja kuangalia na kuona namna ya kutengeneza mtaro, hata kwa kutenga fedha za dharura ili wananchi waondokane na kero hii" alisema Mhe. Mangosongo.
Wilaya ya Mafia ina jumla ya mabwawa 59 ambayo yamekuwa yakizalisha mbu kwa wingi na kupelekea kuenea kwa maambukizi ya malaria, hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imepokea lita 3000 za viuadudu zenye thamani ya Shilingi Milioni 39.6 kutoka Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti malaria.
Wananchi wa Mafia, hasa wakazi wa maeneo ambayo yamekuwa yakizalisha mbu kwa wingi, wametoa shukrani zao kwa Serikali na kuiomba iboreshe miundombinu ya barabara kwa kuweka mitaro ili maji yasituame katika makazi yao.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.