Kwa kipindi cha robo ya tatu(Januari- Machi) mwaka fedha 2020/2021 tarehe 29/04/2021 Kamati ya Fedha, utawala na Mipango ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. Juma Salum Ally ilitembelea miradi mitano ya Halmashauri iliyopo Tarafa ya Kaskazini kama ifuatavyo;-
1. Zahanati ya Kijiji cha Gonge.
Zahanati iko hatua ya umaliziaji kwa kupaka rangi na kuingiza umeme, kujenga placenta pit, kichomea taka na nyumba ya watumishi. Kamati ilikuta kazi ya umaliziaji inaendelea. Kamati iliridhishwa na hatua iliyofikiwa na ilishauri menejimenti iweke mikakati ya kuhakikisha zahanati inapokamilika ipate mahitaji kama samani, vifaa tiba na watumishi angalau wachache kwa kuanzia.
2. Zahanati ya Kijiji cha Kifinge.
Kazi ya umaliziaji inaendelea aidha bado placenta pit, kichomea taka na nyumba ya watumishi havijajengwa. Wajumbe walishauri mifuko ya saruji iliyoazimishwa shule ya msingi Kifinge irejeshwe ili kukamilisha ujenzi uliosalia ikiwemo nyumba ya watumishi. Wajumbe walishauri sehemu ya mbele ya jengo la zahanati kimwagwe kifusi kudhibiti adha ya maji na tope. Mheshimiwa diwani kata ya Baleni aliwathibitishia wajumbe kuwa suala la kifusi liko ndani ya uwezo wao watakamilisha. Kamati iliridhishwa na hatua iliyofikiwa na ilishauri menejimenti iweke mikakati ya kuhakikisha zahanati inapokamilika ipate mahitaji kama samani, vifaa tiba na watumishi angalau wachache kwa kuanzia.
3. Kituo cha Afya Kirongwe
Wajumbe walisema kuwa gharama zilizotumika kujenga kituo ni kubwa lakini huduma zinazotolewa hazishawishi wagonjwa kutibiwa hapo. Sababu ni upungufu wa watumishi, vifaa tiba na miundombinu mingine. Walishauri Halmashauri itafute namna ya kuhakikisha Kituo kinapata mahitaji yote muhimu ili kitoe huduma bora za tiba.
Pia suala la usafi lilionekana kuwa kero maana kituo kimejaa nyasi zisizofyekwa. Hivyo kamati ilishauri Halmashauri ya Kijiji cha Kirongwe iweke utaratibu wa kufanya usafi kwa kushirikiana na kamati ya usimamizi wa kituo hicho.
4. Zahanati ya Kijiji cha Jimbo.
Pamoja na mwonekano wa jengo kuwa imara, wajumbe walijionea mpasuko wa ukuta uliosababishwa na asili ya udongo wa eneo hilo. Hivyo walitaka kujua utaratibu ukoje kuhakikisha zahanati inafanyiwa marekebisho na inafanya kazi. Akifafanua juu ya hatua zilizopo Kaimu Afisa Mipango (W) alisema tayari milioni 50 zimeshatengwa kwa ajili ya kukamilisha kazi zote ili jengo lifanye kazi. Kaimu mhandisi Ujenzi aliongezea kuwa milioni 50 zikiingia zitatosha kuhakikisha jengo linakamilika na kuanza kutumika.
Kamati ilimwelekeza Mkurugenzi Mtendaji (W) kuhakikisha kuwa ndani ya mwezi wa tano 2021 fedha iwe imepelekwa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo.
5. Eneo la Mwalo na Mnada katika Kijiji cha Bweni.
Wajumbe walikagua eneo la mwalo lililopendekezwa kujengwa mnada wa samaki katika kijiji cha Bweni. Kaimu mwandisi ujenzi aliwataarifu wajumbe kuwa kwa kuanzia zikipatikana milioni 5 kazi itafanyika na mnada utaanza. Wajumbe waliridhia na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji (W) kuendelea na ujenzi wa banda la mnada ili kudhibiti utoroshwaji wa mapato na kuongeza mapato kwa wananchi, kijiji na Halmashauri.
Mwenyekiti wa Halmashauri alihitimisha kwa kuwashukuru wajumbe na kupongeza jitihada zinazoendelea kufanyika katika kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuchochea ongezeko la mapato na huduma bora kwa jamii ya watanzania.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.