Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia, Olivanus Thomas kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya awataka Wakazi wa Mafia kuchukua tahadhari dhidi ya maafa yanayosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.
Maelekezo hayo yametolewa Aprili 14, 2024 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia, Olivanus Thomas kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya alipotembelea maeneo yaliyoathirika na mvua kwa kata ya Kanga, kijiji cha Bweni.
Akiwa ameambatana na kamati ya maafa ya Wilaya, alipata nafasi ya kuongea na wananchi na kuwapa pole kwa maafa waliyoyapata pamoja na kushirikiana nao katika zoezi la kuchimba mtaro ili kuondoa maji kwenye maeneo ya makazi.
"Tumefika hapa kuwapa pole lakini pia kushirikiana kuona namna bora ya kuepusha maafa, haya majanga ni ya kwetu sote haijalishi sisi ni viongozi ila ni sehemu ya wananchi wa hapa, hivyo inabidi tutengeneze mtaro wa dharura kuyaondosha maji haya yasilete madhara zaidi. Pamoja na jitihada zote hizi, kila mwananchi inabidi achukue tahadhari kuepusha madhara makubwa yanayoweza tokea" alisema Ndugu Olivanus.
Maeneo mengine yaliyoathirika na mvua ni pamoja na kata ya Ndagoni, kijiji cha Chunguruma, Kilindoni kwa maeneo ya Bondeni Pwani na Msufini.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.