Kikao cha Baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Mafia cha kupitia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kilifanyika siku ya tarehe 14/06/2021 katika ukumbi wa Magereza.
Katika kikao hicho alishiriki pia Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge , Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Mhandisi Mwanasha Tumbo pamoja na mwakilishi kutoka ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali mkoa wa Pwani.
Mhe. Abubakari Kunenge Mkuu wa Mkoa wa Pwani aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kupata hati safi pia aliwataka kufunga hoja za ukaguzi kabla hazijafika kwenye hatua ya kutakiwa kujieleza ili kuepuka kuzalisha hoja zaidi.
Mkuu wa Mkoa amewataka watumishi kufuata taratibu, kanuni na kuheshimu sheria za utumishi wa umma na kuwasilisha nyaraka za matumizi yote ya Fedha zinazohitajika wakati wa ukaguzi ili kuepuka kuzalisha Hoja.
Nukuu "Sitopenda kuona hoja zinaongezeka na kujirudia kwa mwaka ujao" alisema Kunenge
Pia ameitaka Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato, kusimamia ukusanyaji wa mapato na pia kudhibiti matumizi.
Alitoa rai pia kwa Viongozi wote wa Kisiasa na Kitaalamu Wilayani kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao na kuwaasa wafanya maamuzi kupokea ushauri wa kitaalam ili wafanye maamuzi sahihi.
Alieleza kuwa amekuja kufanya kazi Mkoa wa Pwani na kuwataka wataalamu wote Mkoani hapo kuandaa taarifa yenye Fursa zote muhimu katika sekta zilizopo Mkoani hapo ikiwemo vyanzo vya Mapato, Huduma za Kijamii, Viwanda Kilimo, Biashara, Utalii, Uvivu ili kupata hali ilivyo kwa sasa na kuainisha maeneo yote yanayohitaji maboresho.
Kupitia Taarifa hiyo inayooenesha fursa mbalimbali katakuwa na Siasa nzuri ya kiuchumi ya kutumia kidogo kupata kingi na kwa kuvifanyia kazi vipaumbele hivyo muhimu kutaleta maendeleo ya haraka ya Wilaya na Mkoa kwa ujumla.
Pia aliongezea kwa kusema kuwa kuwa ili kuleta maendeleo ya haraka katika wilaya ya Mafia ni lazima viongozi na wafanyakazi kuondokana na dhana ya kuwa '' Mafia ni eneo la pembezoni lililotengwa na kutothaminiwa bali kuanza kuinadi upya Wilaya ya Mafia''.
Akieleza kuhusu changamoto ya uhaba wa watumishi, Taa kwenye Kiwanja cha Ndege, Tozo kwa mizigo na magari mara mbili kwenye Bandari ya Nyamisati na Kilindoni mafia amesema ameyachukua na atayafanyia kazi.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Kunenge alipokea taarifa ya Wilaya na pia alipata fursa ya kuzungumza na Baraza la Madiwani na Kutembelea Kiwanda kikubwa cha kuchakata Samaki cha TANPESCA Ltd.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.