Kituo cha Afya cha Kirongwe kimezindua rasmi huduma ya upasuaji kwa kina mama, leo Februari 18, 2025 ambapo upasuaji uliofanyika kwa mama mjamzito umekamilika salama.
Kituo hicho kilichoanza kutoa huduma za afya tangu mwaka 2020 hakikuwahi kuwa na huduma ya upasuaji kutokana na sababu mbalimbali ambazo ziliwalazimu wananchi kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wialya.
"Kwa kuanzisha huduma hii hapa, tumewasogezea wananchi huduma karibu zaidi. Tunashukuru Serikali kwa kutuongezea rasilimali watu wakiwemo madaktari na wahudumu wengine, pamoja na kutuboreshea miundombinu kama majengo, jenereta, na vifaa mbalimbali ambavyo mwanzo vilikuwa sababu ya kutokuwa ha huduma hii" ameeleza Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya, Ndg. Omary Mvoulana.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Kirongwe Mhe. Said Msabaha ameishukuru Serikali kwa kuendelea kujali wananchi hasa katika sekta ya afya.
"Leo tumeanza kwa mama wa kwanza kujifungua salama, tunashukuru madaktari na wauguzi kwa hatua hii na tunapongeza jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha huduma za afya, hasa kwa mama na mtoto, zinaboreshwa" amesema Mhe. Msabaha.
Akitoa shukrani zake baada ya kufanyika upasuaji, Kassim Hassan ambaye ni mume wa mzazi aliyejifungua mtoto wa kike, ameeleza hatua kubwa iliyofikiwa baada ya wananchi kupitia changamoto hapo awali.
"Nashukuru mke wangu amejifungua salama, mwanzo nililazimika kumpeleka Hospitali ya Wilaya kujifungua mtoto wetu wa kwanza, lakini leo huduma hii ameipata hapa, tunamuomba Mungu awajalie viongozi wetu ili watuletee huduma kama hizi karibu yetu" alieleza Bw. Hassan.
Hatua hii itasaidia kupunguza kero ya msongamano katika Hospitali ya Wilaya na kuleta mabadiliko chanya katika suala la afya ya mama na mtoto, ikiwemo kuokoa maisha yao pindi changamoto zinapotokea.
" Tulikuwa tukisafiri kwa shida kufuata huduma Hospitali, ilikuwa shida kipindi cha masika na hali ya barabara si nzuri, baadhi ya wanawake walikuwa wakijifungua njiani, ila sasa tunaishukuru Serikali kwa maendeleo haya" alisema Aisha Ahmad, mkazi wa kitongoji cha Shalaza.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.