Taasisi ya KOFIH imekabidhi rasmi mradi wa jengo la mama na mtoto kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia leo Agosti 28, 2025.
Makabidhiano hayo yaliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya yameshuhudiwa na baadhi ya wataalam kutoka shirika hilo, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mafia, pamoja na wataalam wa Idara ya afya wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndugu Mussa Kitungi.
Akikabidhi mradi huo, Mwakilishi wa KOFIH nchini Tanzania Bw. Gyeongbae Seo amefurahishwa na juhudi za Serikali pamoja na uongozi wa Halmashauri kuhakikisha mradi unafikia hatua nzuri ambayo itawezesha wananchi kupata huduma bora.
" Tunapongeza jitihada za Halmashauri kuchangia pale ambapo tuliishia sisi na kuhakikisha inaonesha umiliki wa mradi huu. Jengo hili halitohudumia kina mama na watoto wakati huu yu, bali hata vizazi vijavyo" alieleza Bw. Seo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mercy Mtaita ameishukuru taasisi ya KOFIH kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha afya ya mama na mtoto na kusisitiza juu ya utunzaji wa miundombinu iliyopo ili iweze kusaidia kina mama wengi wa Mafia na kupunguza rufaa nyingi za wananchi kwenda kutibiwa nje ya wilaya.Aidha, amewataka wahudumu wa afya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia miongozo iliyopo.
" Tutoe huduma kulingana na miongozo iliyowekwa tukiamini kwamba hata Mungu anatuona, tunaweza tusilipwe hapa duniani ila Mwenyezi Mungu akiangalia kazi tuliyofanya basi tutapewa thawabu zetu" alisisitiza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Ndugu Mussa Kitungi ameahidi kuwa Halmashauri itaitunza miundombinu iliyopo pamoja na kuhakikisha kuwa huduma inaimarishwa ili wananchi wapate kunufaika kama ilivyokusudiwa.
" Kutekelezwa kwa mradi huu kunadhihirisha ni kiasi gani Serikali inashirikiana vyema na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, hivyo kukamilika kwa jengo hili kutaboresha huduma za afya wilayani" alieleza Ndugu Kitungi.
Taasisi ya KOFIH ilichangia kiasi cha Shilingi Milioni 270 katika utekelezaji wa mradi huo, huku Serikali ikitoa kiasi cha Shilingi Milioni 300 ili kuhakikisha jengo la mama na mtoto linakamilika.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.