Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo amewataka watumishi kuwa waaminifu kwa kufuata miiko ya kazi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii katika kutumikia wananchi maana Serikali ipo nao sambamba kuhakikisha inaboresha maslahi yao.
Mhe. Mangosongo ameyasema hayo leo Mei 01, 2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Kimataifa, Mei Mosi ambayo kiwilaya imefanyika katika viwanja vya ofisi za Halmashauri, Chicco.
Ameeleza kuwa Serikali chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa watumishi kwa kuleta fedha za kujenga makazi, shule na vituo vya kutolea huduma ya afya pamoja na kuajiri watumishi wapya.
Akijibu risala iliyosomwa kutoka kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi, amesema kuwa Kwa mwaka ujao wa fedha, 2025/2026 watumishi wapya 147 wametengewa bajeti ya mishahara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia.
Imeelezwa kuwa, maslahi ya watumishi ni jambo ambalo kwa umuhimu wake, Serikali imeendelea kuzingatia kila mwaka kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao.
"Serikali inatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kulipa stahiki za watumishi. Kwa mwaka wa fedha ujao 2025/2026, watumishi 371 wanatarajiwa kupanda madaraja na tayari bajeti yao imetengwa, huku watumishi 11 kubadilishwa muundo" ameeleza Mhe. Mangosongo. Hivyo watumishi endeleeni kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sheria na miongozo" aliongeza.
Aidha, amewataka watumishi kuendelea kujiandaa na uchaguzi mkuu mwaka huu 2025 kwa kuhakikisha kuwa wale wote ambao hawakuandikishwa, wanajitokeza kuboresha taarifa zao mara zoezi hilo litakapoanza kwa mara ya pili Mei 16 hadi 22, 2025.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi mwaka 2025 inasema kuwa " Uchaguzi Mkuu 2025 Utuletee Viongozi Wanaojali na Kuthamini Haki na Maslahi ya Wafanyakazi"
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.