Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Aziza Mangosongo akiwa ameambatana na kamati ya Usalama, uongozi wa Halmashauri pamoja na watumishi, amewaongoza wakazi wa Mafia katika maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika Septemba 26, 2024 katika Shule ya Sekondari ya Baleni.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mangosongo ameeleza namna Serikali ilivyojizatiti kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa wananchi wa rika zote.
Aidha, amewataka wazazi kuwasimamia vyema watoto wao wawapo shuleni na nyumbani ili wazingatie elimu na kuepusha tabia za utoro pamoja na matendo yasiyofaa ambayo hupelekea ukatili wa kijinsia.
"Hatuwezi kukubali watoto wetu kufeli, Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan analeta fedha nyingi ili wanafunzi wasome na wafaulu, natamani wazazi tuwalee watoto wetu kwa ubora kama sisi tulivyolelewa" alisema Mhe. Mangosongo.
Katika kuhakikisha elimu inaimarika, mwaka 2021 Serikali ilianzisha miradi mbalimbali ikiwemo SEQUIP na MEMKWA ambayo imewasaidia wasichana na wavulana walioacha shule kutokana na changamoto mbalimbali waweze kurejea kwenye masomo.
Mariam Juma ni mmoja wa wanafunzi wa kidato cha tano walionufaika na miradi hiyo kwa kumuwezesha kurudi shule baada ya kupata changamoto zilizopelekea kukatisha masomo yake.
" Nilianza elimu ya watu wazima mwaka 2022, nilihamasika kujiunga na elimu hii baada ya kumsikia Mhe. Rais akitutaka turudi shuleni" alisema Mariam. " Nilikata tamaa kabisa baada ya kukumbwa na changamoto, nilipata nafasi kuanza masomo na baada ya kufanya mtihani wa kidato cha nne nilifaulu na kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano katika shule ya Sekondari Kitomondo, nawaomba mabinti wenzangu wasikate tamaa na warudi shuleni kutimiza malengo yao" aliongeza.
Kwa sasa, Halmashauri kupitia Idara ya Elimu Sekondari imeanzisha darasa la wanafunzi 19 wa elimu ya watu wazima na kuendelea kutoa hamasa kwa jamii ili kuhakikisha wanatekeleza na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha elimu.
" Kupitia programu hii, nimeweza kugundua mambo mengi ambayo yanaweza kufanyiwa kazi na kutufikisha mahala ambapo Taifa, Mikoa na Halmashauri yanatarajiwa kufikiwa, ikiwemo kuhamasisha wanafunzi wote wa kike na wa kiume walioacha shule kurudi shule kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao" alisema Hawa Said, mratibu wa Kitengo cha Elimu ya Watu Wazima.
Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima kwa mwaka 2024 yameongozwa na kauli mbiu isemayo " Ujumuishi katika Elimu Bila Ukomo kwa Ujuzi, Ustahimilivu, Amani na Maendeleo"
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.