Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Aziza Mangosongo amezindua rasmi mafunzo kwa wataalam wasimamizi wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa katika Makundi ya Wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu.
Mafunzo hayo yameanza tarehe 26 Septemba, 2024 na yanatarajiwa kutamatika tarehe 4 Oktoba, 2024 ambapo elimu hiyo itatolewa kwa Makundi mbalimbali wakiwemo wataalamu wa Maendele ya Jamii, Kamati za huduma za mikopo ngazi za kata, Kamati ya Huduma za Mikopo ya Halmashauri, Kamati ya Uhakiki wa Mikopo ngazi ya Wilaya, Waheshimiwa madiwani na Timu ya Menejimenti ya Wilaya.
Wataalamu, viongozi na Wanakamati watapata maelekezo juu ya usimamizi na utekelezaji wa Mwongozo mpya na Kanuni za utoaji wa mikopo za mwaka 2024.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhe. Mangosongo amewataka maafisa maendeleo kuhakikisha kwamba wanasimamia haki pamoja na kuwa waadilifu ili kurahisisha utoaji wa mikopo mara tu mikopo hiyo itakapoanza kutolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndugu Mussa Kitungi ameahidi kusimamia vyema upatikanaji wa mikopo na kuwasisitiza wasimamizi wa mikopo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na misingi ya uadilifu, haki na usawa.
Serikali imeandaa muongozo mpya wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao utatumika kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa kuhusu utoaji na upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10, ili kwa kuzingatia vigezo na masharti, wapate kunufaika kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.