Wananchi wa Wilaya ya Mafia wanatarajia kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa umeme kupitia mradi mkubwa wa Gridi ya Taifa utakaosaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Mradi huo utahusisha kupitisha waya chini ya maji kwa urefu wa KM 70 na kina cha KM 1.5 kutoka Kisiju wilayani Mkuranga hadi Mafia, ambapo utapitishwa kwa urefu wa KM 6.5 kutoka fukweni, Tereni hadi Kichangachui.
"Tunaamini mradi huu utakuwa mwarobaini kwa tatizo la umeme wilayani Mafia, hivyo nawaomba tutoe ushirikiano kwa Serikali ili kufanikisha hatua hii" alisema Ndugu Jovinus Kyaruzi, Afisa Tawala wilaya ya Mafia katika mkutano uliofanyika eneo la Kigamboni, Mei 15, 2025.
Mradi huo unatarajiwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa Serikali tofauti na hali ilivyo sasa ambapo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani Mafia limekua likitumia gharama kubwa kununua mafuta ya kuendesha mitambo.
" Tunajaribu kupunguza gharama za uzalishaji wa umeme kwa kutumia gridi yaTaifa, maana tunatumia gharama kubwa kununua mafuta ya 'generator' hapa Mafia, gharama tutakazo okoa zitatumika kufanya shughuli nyingine za maendeleo " alisema mpimaji ardhi kutoka TANESCO, Ndugu Jafari Lindonde.
Akijibu swali lililoulizwa na mwananchi kuhusu ulipwaji wa fidia , Mthamini wa Wilaya ya Mafia Ndugu Philip Kubingwa ameeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria za ardhi, miradi kama hii inaanza kwanza fidia na baadaye mradi kuendelea ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Mhe. Juma Salum ameipongeza Serikali kupitia TANESCO kwa kuja na suluhisho la upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wakazi wa Mafia ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
"Sisi maslahi yetu makubwa kwenu ni kuhakikisha anayestahili kulipwa fidia, analipwa . Tunawashukuru kwa kuupokea mradi huu ili na sisi wananchi wa Mafia tuunganishwe kwenye gridi ya Taifa na kuweza kufanya shughuli zetu za kiuchumi" alieleza Mhe. Salum.
Madi huu unahusisha upimaji shirikishi ambapo wananchi wanashirikishwa katika upimaji wa maeneo kabla ya kuanza kwa mradi.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.