Wilaya ya Mafia, leo Machi 22, 2025 imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Misitu pamoja na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa kwa kupanda miti 1500 katika chuo cha VETA kilichopo kata ya Ndagoni.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo amezitaka taasisi zote zilizo za Serikali na zisizo za serikali pamoja na wananchi kuwa mstari wa mbele katika kutunza mazingira kwa kuepuka kukata miti kiholela pamoja na kuzingatia matumizi ya nishati safi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Ndugu Abdul Haji Faki, amesema kwamba zoezi la upandaji miti ni endelevu huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kuchukua miti hasa msimu huu wa mvua.
Kwa mwaka huu 2024/2025, miti 363,500 imepandwa wilayani Mafia ikiwemo mikoko ambapo lengo ni kufikisha miti 500,000 mpaka kufikia mwezi Juni, 2025.
Katika hatua nyingine ya utunzaji wa mazingira, Wakala wa Huduma za Misitu wilayani Mafia (TFS), imeomba kupatiwa eneo la Hekari 30 kwa ajili ya shuguli za uhifadhi ikiwemo ufugaji wa nyuki.
Kauli mbiu ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa ni "Ongeza Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali kwa Kizazi hiki na Kijacho".
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.