Wakazi wa Mafia wameadhimisha Siku ya Usafi Duniani kwa kusafisha fukwe katika kitongoji cha Tumbuju kilichopo kata ya Ndagoni pamoja na eneo la Soko Mjinga lililopo Kilindoni.
Zoezi hilo limeongozwa na Kitengo cha Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira,serikali ya kata na kijiji, BMU, kwa kushirikiana na vyombo vya usalama, kikundi cha Takataka Dampo kilichopo wilayani, na vikundi vya michezo (jogging).
Akitoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi wa mazingira, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Taka na Usafi wa Mazingira, Bwana Othman Masanga, amesisitiza umuhimu wa kufanya usafi kila siku kwa ajili ya kulinda afya na kutokomeza magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wao, wakazi wa kitongoji cha Tumbuju wameishukuru Serikali kupitia uongozi wa Halmashauri kwa kuhamasisha na kusimamia usafi, ambapo wameahidi kutoa ushirikiano ili kuboreaha mazingira yao ya biashara na makazi.
" Tumefurahi kuwa pamoja na viongozi wetu leo kwa kufanya usafi, tunaomba waendelee kuwawajibisha wasiozingatia usafi bila kuogopa ili fukwe zetu ziwe safi" alisema Mtoro Kimbau, mkazi wa Tumbuju.
Wananchi zaidi ya 80 wamejitokeza kufanya usafi katika fukwe, ambapo zaidi ya Tani moja ya taka zimekusanywa.
" Kwetu kama wadau wa mazingira, tumefurahi sana kwa ushirikiano mkubwa tuliopata na tunawaomba wananchi kuendelea kuongeza nguvu kutunza mazingira yetu" alisema Abdu Amrani, Mwenyekiti wa Kikundi cha Kijamii cha Takataka Dampo kinachojihusisha na Udhibiti wa taka wilayani Mafia.
Zoezi la usafi kwa kata ya Kilindoni lilihitimishwa na Ndugu Juma Salum mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia.
Siku ya Usafi Duniani kwa mwaka 2024 inaongozwa na kauli mbiu isemayo " Uhai Hauna Mbadala, Zingatia Usafi wa Mazingira".
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.