Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo ameielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuhakikisha inaweka nguvu kubwa katika kusimamia miradi ili kuepuka kuwa na miradi ambayo haitekelezeki kwa wakati.
Mhe. Mangosongo ametoa maelekezo hayo Februari 04, 2025 kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ( DCC) kilocholenga kupitia na kujadili mapendekezo ya Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri pamoja na taasisi mbalimbali.
Ameeleza kuwa miongoni mwa mambo yanayokwamisha utekelezaji wa miradi ni pamoja na wazabuni kuchelewesha vifaa vya ujenzi, kulegalega kwa usimamizi wa miradi na kucheleweshwa kwa fedha za miradi.
" Tunapitisha bajeti lakini kuna changamoto ya wazabuni, kwa kuchelewesha vifaa maeneo ya miradi na hii inapelekea kuleta shida kwa wasimamizi wa miradi na kuwa na miradi viporo" ameeleza.
Aidha, ameelezea mambo mbalimbali ya kuzingatiwa katika uandaaji wa bajeti ya Halmashauri na taasisi ikiwemo kuhakikisha kero ya upungufu wa madawati shuleni inatatuliwa, stahiki za watumishi pamoja na mipqngo ya kutatua uhaba wa watumishi hasa katika sekta ya afya na elimu.
Halmashauri inatarajiwa kuongoza Mkutano wa Baraza la Madiwani siku ya tarehe 6 Februari, 2025 kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za Halmashauri pamoja na kupitia Rasimu ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.