Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo, amekabidhi kiasi cha Shilingi Milioni 41.75 kwa vikundi vitatu ambavyo vinawakilisha vikundi vingi vitakavyopokea mkopo ikiwa ni fedha ya mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri.
Mhe. Mangosongo amekabidhi kiasi hicho leo Novemba 07, 2024 katika hafla fupi ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.
Hatua hii inakuja kufuatia kufunguliwa rasmi kwa dirisha la maombi ya usajili wa vikundi vya asilimia 10 Septemba 27, 2024 na kufungwa rasmi Oktoba 26, 2024 ambapo hadi kufikia Novemba 06 2024, vikundi 424 vilikuwa vimesajiliwa na kati ya hivyo, vikundi 220 vimeomba mkopo.
Mhe. Mangosongo amewataka wananchi wote walioomba mikopo kurejesha fedha hizo kwa wakati pindi watakapopatiwa, kwa kuzingatia mwongozo na taratibu pamoja na kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Juma Salum, amewatoa wasiwasi walioomba mikopo kuwa haki itatendeka kwa walioomba mikopo kwakuwa fedha zinazoombwa zitatoka kulingana na michanganuo ya kibiashara iliyowasilishwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 535.9 kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye ulemavu, ambapo mchakato wa utoaji wa mikopo kwa makundi hayo bado unaendelea.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.