Kiasi cha Shilingi Milioni 466 zinatarajiwa kutolewa kwa vikundi 60 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ikiwa ni mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mafia.
Akikabidhi hundi kwa vikundi vya wanufaika wa mkopo leo Januari 29, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo amesema kwamba Serikali inatarajia wananchi kupiga hatua kubwa kiuchumi baada ya kuwezeshwa kupitia mikopo hiyo kwa wananchi kuhakikisha wanatumia fedha kwa malengo yaliyotarajiwa.
" Ikitokea mmefanya tofauti na malengo ya mikopo hii, mtakuwa mmekwenda tofauti na nia ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kamati ya uhakiki wa mikopo, hivyo hakikisheni mikopo hii inatumika kama ilivyokusudiwa pamoja na kufanya marejesho" alisema Mhe. Mangosongo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Juma Salum amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa katika kufanya biashara zao ikiwemo ulipaji wa leseni za biashara pamoja na ushuru ili wananchi wengine nao waweze kunufaika.
Wanufaika wa mikopo hiyo wametoa pongezi na kuishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya wananchi na kuahidi kuwa watakuwa waaminifu katika marejesho.
" Kabla ya kupata mkopo nilikuwa na msingi mdogo, ila nikapata taarifa kuwa kuna mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri, hivyo nikahamasika kufanya maombi na kufanikiwa kupata na nikarejesha kwa wakati, na hivi sasa nimeomba tena" alieleza Haji Mwarabu, mfanyabiashara wa samaki mwenye ulemavu kutoka kata ya Kanga, kijiji cha Bweni. " Natoa wito kwa wananchi wenzangu kuomba mkopo na kurudisha kwa wakati" aliongeza.
Halmashauri ya Wilaya ya Mafia inatarajia kufungua dirisha la pili la uombaji wa mikopo ya asilimia 10 ifikapo Januari 31, 2025.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.