Watumishi wilayani Mafia wametakiwa kuwa na nidhamu wawapo kazini pamoja na kuheshimu mamlaka zilizopo.
Hayo yamesemwa leo Januari 30, 2025 na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Pwani Ndg. Peter Bila wakati wa Semina kwa Watumishi wa Umma wilayani Mafia iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Chicco.
Ndg. Bila ameeleza kwamba watumishi wana wajibu mkubwa kuzingatia weledi na nidhamu wawapo kazini ili waweze kuwatumikia wananchi ipasavyo pamoja na kutii mamlaka.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Ndg. Mussa Kitungi amepongeza na kutambua mchango mkubwa wa kuwa na semina na mafunzo kwa watumishi ili kuwaongezea ujuzi katika masuala ya msingi wawapo kazini.
Ndg. Kitungi ameeleza kuwa suala la maadili kwa watumishi ni la muhimu kupewa kipaumbele na halina budi kuzingatiwa maana miongoni mwa mambo ya kupambana nayo baada ya ujinga, maradhi na umaskini, suala la maadili ni la msingi.
" Kwa mazingira tuliyonayo kwa sasa, ukiniuliza mimi nitasema maadui wameongezeka, adui wa nne ni ukosefu wa maadili" ameeleza Ndg. Kitungi.
Aidha, ameelezea umuhimu wa kuwepo kwa semina hiyo kila mwaka ili kufundisha suala la maadili na kuahidi kuwa ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano kufanikisha hilo.
Semina hiyo kwa watumishi wa umma imeandaliwa na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za kiserikali zikiwemo taasisi za kifedha.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia, Ndg. Shabani Shabani amepongeza hatua hiyo na kutambua mchango wake katika kuongeza uwezo wa watumishi katika utendaji kazi akitambua mchango wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ( WCF), OSHA, TUGHE, Action Aid, Benki za NMB na CRDB kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.