Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Aziza Mangosongo ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutatua changamoto za walimu zikiwemo madeni ya uhamisho na likizo, pamoja na ukosefu wa nyumba za watumishi.
Mhe. Mangosongo ameyasema hayo katika kongamano la walimu wanawake lililofanyika wilayani Mafia leo Agosti 23, 2024.
" Mlinipa taarifa kuhusu changamoto zenu nyingi ikiwemo madeni ya uhamisho, sasa madeni yenu yatalipwa kwa mkupuo maana Mhe. Rais yupo kazini" alisema Mhe. Mangosongo. Kwa mfano, hapo awali kwa shule za sekondari, madeni ya likizo yalikuwa yakitengewa Milioni 14 kwa mwaka, ila sasa hivi ni Milioni 28 na fedha za uhamisho zilitengwa Milioni 16, ila kwa sasa ni Milioni 40.
Mhe. Mangosongo ametumia fursa hiyo pia kuwasisitiza walimu juu ya weledi katika kazi pamoja na kujituma ili kuleta mabadiliko chanya kwa wanafunzi na sekta ya elimu nchini.
"Niwaombe sana walimu maana tunawajua watoto, hivyo tukashirikiane na wazazi na watoto wenyewe ili kuongeza ufaulu na kupunguza changamoto zinginezo zikiwemo ukatili wa kijinsia, utoro na mengineyo"
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bi.Tabu Makanga ameishukuru Serikali chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupigania maslahi ya walimu kama vile kuwapandisha madaraja walimu wa Sekondari na Msingi.
Kwa mwaka 2024, walimu 174 wamepanda madaraja; ambapo walimu 114 ni walimu wa shule za msingi na walimu 60 wa sekondari huku Halmashauri kupitia Idara ya Elimu Msingi na Sekondari ikiendelea kuhakikisha walimu wengine wanapata maslahi yao kama kupunguza madeni ya likizo na posho.
" Kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024 tumeweza kupunguza madeni ya Milioni 40 kwa walimu wa Sekondari na Milioni 94.86 kwa ajili ya walimu wa shule za msingi" alieleza Bi. Makanga. Miongoni mwa shughuli zilizofanyika katika kongamano hilo ni pamoja na utoaji wa misaada kwa wafungwa pamoja na wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.