Mkuu wa Wilaya ya Mafia ameelekeza kuwa soko la mwani wilayani Mafia ni huru na hivyo Serikali inaruhusu ushindani wa wanunuzi wa zao hilo kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo katika soko bila vipingamizi vya mtu mmojammoja au kampuni.
Mhe. Mangosongo ameyasema hayo leo Oktoba 6, 2025 wakati wa kikao chake na wadau wa mwani wilayani Mafia kilicholenga kujadili na kusikiliza kero za wakulima wa zao hili ili kuweka mikakati stahiki ya kutatua changamoto zilizopo, hasa kuwepo kwa mnunuzi mmoja mkubwa wa zao hilo kisiwani Mafia ambaye ni kampuni ya 'Mwani Mariculture'.
" Sisi kama Mafia tunaenda na azimio la kufungua mipaka ya wanunuzi ili waje kununua mwani Mafia, na kingine tunataka taratibu zifuatwe, chochote kitakachokuwa kinapelekwa kwa wakulima, kipite Halmashauri ili Idara ya Kilimo wakione. Lengo letu wakulima wanufaike na bei kupanda kutoka Shilingi 800 kwa Kilo hadi kufikia Shilingi 1000" alieleza Mhe. Mangosongo akisisitiza ushindani kakika soko la mwani.
Awali, akiwasilisha taatifa ya mwenendo wa zao la mwani, Afisa Uvuvi wa Wilaya Ndugu Alfahad Mohamed alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/ 2025, mavuno ya mwani yalikuwa ni Tani 600 zenye thamani ya Shilingi Milioni 420 kwa bei ya Shilingi 700 kwa kilo huku asilimia 90 ya wakulima wa zao hilo ikiwa ni wanawake.


Kwa upande wake, Mhifadhi Shirikishi Jamii, Hifadhi ya Bahari Mafia( HIBAMA) Ndugu Albert Makalla, ameeleza jitihada za taasisi hiyo katika kuhakikisha wakulima wa mwani wanaongeza thamani ya zao hilo kwa kutoa mafunzo kupitia wataalam mbalimbali ndani ya Wilaya na nje ya Wilaya na kutoa wito kwa wakulima kuchangamkia fursa za mafunzo pale zinapotokea.
Wakulima wa mwani kutoka maeneo mbalimbali wilayani Mafia wameishukuru Serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kuwakutanisha na kuweka mikakati ya kuboresha zao hilo kwa kutatua changamoto wanazokumbana nazo.
" Tunaishukuru Serikali na Ofisi yako kwa jambo hili, ila tunaomba mtusaidie maana tuna changamoto sana ya vitendea kazi pamoja na ujuzi wa kupanda zao hili" alieleza Bi. Rabihu Hemedi, mkulima wa mwani kutoka kijiji cha Banja.
Imebainika kuwa, elimu ni jambo muhimu katika kuhakikisha zao hilo linaboreshwa na kupanda thamani ili kukuza soko lake ambalo halijawa na mwenendo mzuri kama inavyotakiwa pamoja na kuunda ushirika ili kuleta suluhisho.


" Nashukuru sana kwa kikao hiki adhimu na muhimu pia kuweza kumuomba Mkuu wa Wilaya atusaidie kupitia wataalam ili tupate ujuzi kuhusu upandaji mwani, pia tunaomba mchakato wa uanzishwaji wa ushirika ili tuweze kukwamuka" alieleza Bw. Nasri Basha, mkulima wa mwani kutoka kijiji cha Kiegeani.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mangosongo amewataka wataalam kuhakikisha wanapata takwimu sahihi kuhusu wakulima wa mwani waliopo pamoja na hali ya zao hilo kwa ujumla ili kuweka mikakati yenye uhalisia kuboresha zao hilo.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.