Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Zephania Sumaye ameongoza zoezi la kuteketeza shehena mbalimbali za bidhaa ambazo zimepita muda wa matumizi.
Zoezi hilo lililofanyika Febuari 02 limekuja baada ya kubaini mzunguko mkubwa wa bidhaa zilizopita muda ambazo zimekuwa zikiendelea kuwepo madukani.
" Tumekuwa tukitoa rai kwa wananchi na wafanyabiashara mara kwa mara kwamba waangalie kile kinachokwenda kwa ajili ya walaji kiwe kina ubora unaotakiwa, vinginevyo tunahatarisha afya za Watanzania" alisema Mhe. Sumaye. "Serikali haiwezi kufumbia macho kwa kuacha afya za Watanzania ziwe matatani kwa ajili ya watu wachache wanaotaka kujipatia faida binafsi" aliongeza.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Afya wa Wilaya, Elphace Sembeli amesema kuwa ukaguzi uliofanyika Januari 30 mwaka huu ulibaini bidhaa zaidi ya Tani tatu zikiwemo mchele, unga na biskuti ambazo zimeisha muda wake wa matumizi, na kuwataka wafanyabiashara kuwa waangalifu kwa kuhakikisha mzigo unaoingia kisiwani una muda mrefu wa matumizi.
Hatua hii ya kubaini uwepo wa bidhaa zilizokwisha matumizi ni mwendelezo wa oparesheni mbalimbali wilayani zikiwemo za ukomeshaji wa dawa za kulevya na ukomeshaji wa ukatili wa kijinsia na watoto.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.