Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo ameielekeza Wakala ya Barabara Tanzania ( TANROADS) wilayani Mafia kutengeneza mitaro itakayosaidia kuondosha maji ambayo yamekuwa yakituama katika maeneo mbalimbali kwa muda mrefu na kuleta kero kwa wakazi pamoja na kupelekea kuongezeka kwa mazalia ya mbu.
Akitoa maelekezo hayo leo Septemba Mosi, 2025 wakati wa kikao cha kutambulisha msambazaji wa vyandarua ambaye ni Bohari ya Dawa ( MSD), Mhe. Mangosongo ameitaka TANROADS kuhakikisha kuwa inaweka miundombinu mizuri itakayosaidia kumalizika kwa tatizo la maji kutuama hasa katika maeneo ya pembezoni mwa barabara, maeneo ya Hospitali na makazi ya watu.


" Barabara nyingi au sehemu nyingi zina madimbwi ila hatuna mifereji, hivyo madimbwi haya yatengenezewe mifereji ili maji yasituame na kuweza kutengeneza vimelea vya mbu" alisisitiza.
Kwa upande wake, Mratibu wa Malaria wa Mkoa wa Pwani Dkt. Themistocles Nyeme ameeleza kuwa zaidi ya vyandarua 1,200,000 vinatarajiwa kusambazwa mkoani Pwani ikijumuisha halmashauri saba ambazo zina maambukizi makubwa ya malaria ikiwemo wilaya ya Mafia.
Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya malaria wilayani Mafia na mkoa wa Pwani kwa ujumla.
Kiwango cha maambukizi ya malaria mkoani pwani kwa hivi sasa ni asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 14 kwa mwaka 2022.
" Kwa Halmashauri yetu pia, kiwango cha maambukizi ya malaria ni asilimia 6.7, hivyo tunatoa wito kwa wananchi kujikita katika njia mbalimbali za kujikinga na malaria ikiwemo kutumia vyandarua, kuwahi kufika katika vituo vya kutolea huduma ya afya mara tu wapatapo dalili za malaria pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira " alieleza Bi. Rukia Maumba, Mratibu wa Malaria wilaya ya Mafia.
Katika hatua nyingine, wahudumu wa afya wamesisitizwa kuwa zoezi la ugawaji wa vyandarua liende sambamba na utoaji wa elimu kwa jamii juu ya namna bora ya kuzuia maambukizi ya malaria pamoja na kutumia vyandarua hivyo kwa lengo lililokusudiwa. Zaidi ya vyandarua 48,000 vinatarajiwa kusambazwa katika kaya 21,100 zilizosajiliwa wilayani Mafia.


Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.