Wafanyabiashara wa dagaa wilayani Mafia wanatarajia kunufaika na mradi wa uongezaji wa thamani wa bidhaa hiyo utakaosaidia kukuza soko pamoja na kukuza kipato Chao.
Lengo la mradi huo ni kuongeza uelewa na matumizi ya uzalishaji kwa mfumo gatuliwa wa nishati jadidifu ( Jua) ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji, uchakataji, uongeza thamani na kupunguza upotevu wa zao la dagaa na mnyororo wa thamani wilayani Mafia.
" Tulihamasika na kuungana na wadau wengine ili kuja na mradi utakaobadilisha maisha ya wananchi. Hii ni kutokana na kuwepo kwa changamoto kadhaa katika soko la dagaa" alieleza Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania, Dr. Amani Ngusaru. Tuna matumaini kuwa mradi huu utafanya Mafia kuwa sehemu inayoongoza nchini kwa uzalishaji wa dagaa" aliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo amewashukuru wananchi wakiongozwa na Serikali ya kijiji cha Chunguruma ambapo mradi utatekelezwa, kwa kutoa eneo la mradi ili kuhakikisha wafanyabiashara wanaondokana na changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili.
Utekelezaji wa mradi huo utaokoa asilimia 35 ya thamani ya dagaa inayopotea wakati wa uchakataji.
"Mradi huu utatunufaisha na utatufanya tuingie kwenye ushindani mkubwa katika soko kutokana na ubora wa bidhaa zetu. Tumekuwa tukitumia chanja kuanika dagaa, ambapo kipindi cha mvua, tunapata hasara kulinganisha na kipindi cha jua wakati ambao ndoo ndogo ya dagaa inauzwa kwa Shilingi elfu 50 ila kipindi cha mvua, uanikaji wa dagaa unakuwa mgumu kupelekea dagaa kuharibika, hata bei ya ndoo ndogo hupungua na kufika hadi elfu 15" alieleza Hashim Kirama, Mwenyekiti wa CHAWASA, Mafia.
Kisiwa cha Mafia kinazalisha asilimia 40 ya dagaa wote wanaovuliwa katika ukanda wa bahari ya Hindi, hivyo uwepo wa mradi huu utafanya Mafia iendelee kuzalisha dagaa wengi zaidi kutokana na ubora wa uchakataji pamoja na utunzaji wa mazingira.
Mradi huu unatekelezwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani ( WWF) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama mashirika na taasisi za Kiserikali na zisizo za kiserikali ikiwemo WorldFish, TAFIRI Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, FETA), CHAWASA, na wananchi ambao wote kwa pamoja wana mchango mkubwa kuleta maendeleo.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.