Utunzaji wa mazalia ya samaki una manufaa mengi endapo utapatiwa kipaumbele ili unufaishe jamii na kuleta mapato serikalini pamoja na kuinua uchumi wa wananchi.
Kwa kutambua na kuizingatia dhana ya uchumi wa buluu, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) inafanya jitihada za kuelimisha wananchi umuhimu wa uhifadhi wa bahari kwa shughuli za kiuchumi.
Kijiji cha Jojo kilichopo wilayani Mafia ni sehemu mojawapo ambapo wananchi wanaelewa umuhimu wa kutunza miamba ili kupata mazalia mengi ya pweza. Zaidi ya kilo 2150 za pweza zimevuliwa katika kijiji hicho, uvunaji ambao utaleta mafanikio mazuri kiuchumi.
"Zaidi ya asilimia 78.8 ya mapato kwa mwaka 2022/2023 wilayani Mafia imetokana na mazao ya bahari, ambapo Bilioni 1.3 zimekusanywa, hivyo ni muhimu kwetu kuitunza miamba na mazingira kwa ujumla ili tuone umuhimu wa dhana ya uchumi wa buluu" alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Mwl. Kassim Ndumbo.
Shirika la Uhifadhi wa Mazingira duniani (WWF) limekuwa likitoa elimu kwa jamii kutunza miamba ya mazalia ambapo kila baada ya miezi mitatu wananchi wanahamasishwa kutovua ili mazalia yapate kuongezeka.
Utunzaji na uhifadhi wa mazingira ni muhimu kwa rasilimali endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho katika kukuza uchumi wa wananchi na taifa kiujumla, hivyo natoa wito kwa wananchi wa Jojo na Mafia yote kwa ujumla kuhifadhi na kutunza bahari yetu" alisema Japhet Masigo, Mratibu wa Shirika la WWF wilaya ya Mafia.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.