Wito umetolewa kwa wahudumu wa afya kuweka mkazo katika utoaji wa elimu kwenye jamii kuhusu umuhimu wa mama wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wakati pamoja na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Wito huo umetolewa leo Mei 29, 2025 wakati wa kikao cha kujadili viashiria vinavyosababisha vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa lengo la kuweka mikakati ya kuondokana na tatizo hilo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ndagoni Mhe. Mohammed Rashid amewataka wataalam wa afya kuongeza nguvu katika kutembelea jamii ili waweze kutoa elimu kuhusu afya ya uzazi.
" Tumeona tatizo jubwa zaidi ni elimu, elimu ya kutosha haijaifikia jamii hasa kina mama ili kujua umuhimu wa kuhudhuria kliniki mapema na kwenda na mwenza" ameeleza Mhe. Rashid. " Hivyo kwa pamoja tumekubaliana kuwa wataalam washuke kwenda kuwapa elimu ya kutosha kuhusu elimu hii pamoja na kuweka wazi Sera ya afya kuhusu utoaji wa huduma za afya kwa mama wajawazito na watoto wachanga" aliongeza.Akieleza hali ya afya ya uzazi wilayani, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wilaya ya Mafia Bi. Mwanahawa Kassim amesema kwamba changamoto kubwa inayopelekea vifo vya wazazi na watoto wachanga ni kuchelewa kuanza kliniki kwa wajawazito pamoja na wajawazito kutojifungulia vituoni.
"Kwa kipindi cha kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka huu, tumepata wajawazito wapya 686, lakini waliowahi kliniki ni 86 tu ambao ni asilimia 12.5 ambayo ni mbaya sana na lengo la Taifa ambalo linataka asilimia 95 ya wajawazito kuwahi kliniki" alieleza Bi. Kassim
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanaume kuwajibika kwa kuhakikisha wanawapeleka wenza wao kliniki pindi wanapopata ujauzito ili elimu italowayo vituoni iwafikie wote na kusaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kati ya wajawazito waliofika kituoni kwa kipindi hicho ( Januari - Aprili), wajawazito waliosindikizwa na wenza wao ni 445 ambao ni sawa na asilimia 64.8 ambayo ni chini ya lengo lililokisudiwa la kufika asilimia 95.
" Kwa upande wa jamii, naomba nitoe rai kwa kina mama wajawazito kujitahidi kufika kliniki mapema wakiwa na wenza wao ili kupata elimu kuhusu hali za hatari na namna ya kukabiliana nazo, pia kwa Serikali nawaomba watutengenezee miundombinu maana barabarq zikipitika vizuri, mama wajawazito watafika hospitali kwa wakati" alisema Bi. Neema Boaz, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Banja.
Katika kipindi cha miezi minne, Januari hadi Aprili 2025, kati ya wazazi 487 waliojifungua, 10 wamejifungulia njiani ambao ni sawa na asilimia mbili (2), huku changamoto nyingine ikiwa ni saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake inayopelekea vifo kwao.
Kwa kipindi cha miezi minne, wanawake 65 tu walijitokeza kupima saratani ya mlango wa kizazi ambayo ni asilimia 29 ya wazazi, tatizo ambalo wataalam wa afya wameendelea kutoa wito kwa kina mama kufanya vipimo mapema ili kuzuia hatari zinazoweza jitokeza pindi wanapokutwa na matatizo ya saratani pamoja na maambukizi mengine kama Virusi Vya UKIMWI.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.