Serikali kupitia Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA) imeendelea kuboresha huduma ya upatikanaji maji wilayani Mafia kwa kufika asilimia 77.
Hayo yameelezwa na Meneja wa RUWASA wilaya ya Mafia Mhandisi Clement Lyoto wakati wa kikao cha wadau wa maji kilichofanyika Julai 24, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Chicco.
Kikao hicho kilicholenga kujadili hali ya upatikanaji wa maji kisiwani, mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/ 2024 na matarajio ya bajeti ya mwaka 2024/ 2025 kilikutanisha wadau toka taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali, viongozi wa Wilaya, Halmashauri, kata na vijiji, watoa huduma ya maji ngazi ya jamii ( CBWSO) na wananchi.
" Kwa sasa upatikanaji wa maji umefika asilimia 77 na tuna miradi 7 ambayo mingi kati ya hiyo ipo hatua za ukamilishaji, miradi miwili kati ya hiyo tunatarajia kuikamilisha mwezi huu" alieleza Mhandisi Lyoto. " Kwa lengo lile la kufika asilimia 85 kwa 2025, sisi tunategemea kuwa na asilimia 91 kwa vijijini na asilimia zaidi ya 95 kwa mjini" aliongeza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafia na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar Kipanga amemshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza na kutekeleza mahitaji ya wakazi wa Mafia pamoja na kushauri kuunganishwa kwa vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii ( CBWSO) ili kurahisisha utendaji.
Wilaya ya Mafia ina jumla ya vyombo 12 vya watoa huduma ya maji ambapo inatarajia kuwa na vyombo vinne baada ya kuviunganisha.
" Tuna Imani baada ya kuunganishwa vyombo hivi, itarahisisha utendaji kazi wetu na kuwafikia wananchi kwa wakati. Tunaomba kuongezewa uwezo ili tutumikie wananchi" alisema Bw. Yohana, katibu wa CBWSO kata ya Miburani.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.