Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo ameitaka Halmashauri kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wafugaji na wakulima.
Mhe. Mangosongo ametoa agizo hile leo Septemba 24, 2025 akiwa eneo la Kibaoni kata ya Kiegeani wakati wa hafla ya uhamasishaji wa utoaji wa chanjo kwa mafugo ambapo chanjo zilizotolewa ni pamoja na chanjo ya homa ya mapafu kwa ng'ombe, sotoka kwa mbuzi na kondoo pamoja na chanjo ya kideri au mdondo, ndui na mafua ya kuku kwa kuku wa kienyeji.
Mhe. Mangosongo ameeleza kuwa ni muhimu kwa wafugaji na wakulima kuishi kwa amani na upendo na njia mojawapo ya kuhakikisha migogoro inatoweka ni kwa wafugaji kuwa na maeneo maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.


" Ni vyema zaidi wafugaji waandaliwe maeneo maalum kwa ajili ya maeneo ya malisho wasiwe kama wametelekezwa na kupelekea mifugo yao kuzagaa maeneo ya mjini na katika mashamba ya watu" alieleza.
Aidha, amewataka wafugaji pamoja na jamii kwa ujumla kuwa makini kwa kutoshiriki katika tabia ya wizi wa mifugo ambayo ni kinyume na sheria ambapo ameeleza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayejihusisha na wizi wa mifugo.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wafugaji kuwa na zizi la mifugo katika maeneo yao ili kuepusha wizi, mifugo kuingia katika mashamba ya wakulima pamoja na kusambaa kwa mifugo , huku akiwataka maafisa ugani kufanya ukaguzi kuhakikisha agizo linatekelezwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Seleman Kataga ametoa wito kwa wafugaji kujitokeza katika zoezi hilo la chanjo ili kudhibiti milipuko ya magonjwa na kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao ya mifugo yenye ubora.


Zoezi la chanjo kitaifa linakwenda sambamba na zoezi la utambuzi wa mifugo kielektroniki ambapo Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 216 kipindi cha 2025/2026 zinazofanikisha Serikali kuchangia nusu ya gharama ya chanjo hizo.
Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imepokea kiasi cha dozi 49,600 za chanjo zote ikiwa dozi 40,000 ni chanjo za kuku, dozi 8,000 za ng'ombe na dozi 1,600 za mbuzi na kondoo ambapo hadi kufikia sasa kuku 36, 137 wamechanjwa ikifikisha asilimia 90 ya uchanjaji wa kuku, huku zoezi la uchanjaji wa ng'ombe linaendelea ambapo ng'ombe 117 wamechanjwa.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.