Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo amewataka wawekezaji pamoja na wataalam katika taasisi mbalimbali za Kiserikali na zisizo za kiserikali kuhakikisha kwamba wanazingatia maslahi ya wananchi kabla na wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika jamii.
Mhe. Mangosongo ameyasema hayo wakati wa baraza la biashara lililofanyika Machi 26, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ambapo wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji pamoja na wataalam wa Halmashauri na taasisi mbalimbali walishiriki.
"Wawekezaji tunawapenda sana ila tusiwasahau wananchi, tuyaweke maslahi ya wananchi mbele" alisisitiza Mhe. Mangosongo akielezea maeneo ambayo mara nyingi huumiza wananchi kutokana na mikataba ya uwekezaji kutozingatia mahitaji ya msingi ya wananchi hasa masuala ya ardhi.
Pamoja na mambo mengi yaliyojadiliwa na wadau wa biashara na uwekezaji wilayani, masuala ya usafiri wa uhakika yametiliwa mkazo ambapo Serikali kupitia mamlaka husika imeendelea kuchukua hatua kutatua changamoto kwa kuweka mikakati mizuri ikiwemo kuboresha usafiri wa majini kwa kurekebisha MV Kilindoni pamoja na kutengeneza meli mpya inayotarajiwa kukamilika hivi karibuni huku jitihada madhubuti zikkiendelea kuhakikisha usafiri wa anga unaboreshwa kwa kuweka taa katika uwanja wa ndege pamoja na kutanua uwanja.
Uboreshaji wa usafiri utasaidia shughuli nyingi wilayani Mafia kuimarika, hasa uchumi wa buluu ambao umekuwa ukikuza kipato kwa mwananchi mmoja mmoja, Wilaya na Taifa kwa ujumla kupitia utalii, biashara na uwekezaji katika mazao ya bahari, pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma za jamii hasa afya.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.