Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wilayani Mafia ( VETA) kimeandaa mafunzo ya ujasiriamali kwa mama lishe na baba lishe wa kata ya Kilindoni yenye lengo la kuwaongezea ujuzi katika masuala mbalimbali yatakayowasaidia kuboresha biashara zao.
Akifungua mafunzo hayo Juni 17, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo ametoa pongezi kwa chuo cha VETA kwa kuandaa mafunzo hayo na kueleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wajasiriamali ili kuwawezesha katika masuala ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA wilaya ya Mafia Ndugu Salim Jumbe ametoa wito kwa wananchi kujitokeza pindi mafunzo mbalimbali yanapoendeshwa ili waweze kupata mbinu mpya na sahihi ambazo zitawasaidia kukuza biashara zao.
" Tumekuwa tukiendesha mafunzo mbalimbali kwa makundi tofauti kama vile waendesha bodaboda, mafundi ujenzi na waongoza utalii katika chuo chetu, natoa wito kwa wananchi hasa vijana kuchangamkia fursa za mafunzo yanayotolewa na VETA kwa kushiriki kozi za muda mrefu au muda mfupi" alieleza Ndugu Jumbe.
Washiriki wa mafunzo hayo wamekishukuru chuo cha VETA kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo wanaimani yataleta mabadiliko katika shughuli zao za kutafuta kipato.
" Naishukuru sana Serikali kwa kutuandalia mafunzo, tumekuwa tukiona wenzetu wa bodaboda wakipewa mafunzo ila sasa hivi na sisi tumefikiwa, natoa wito kwa kina mama wenzangu kujitokeza ili tushiriki wote" alisema Moza Kazumari, mama lishe kutoka Kilindoni.
Mada mbalimbali zinatolewa ikiwemo masuala ya afya kwa kuzingatia usafi kwenye biashara, mada kuhusu utunzaji wa mazingira, ujasiriamali pamoja na umuhimu wa kuzingatia lishe bora.
Washiriki zaidi ya 200 wanatarajia kunufaika na mafunzo hayo yanayoendeshwa kwa siku tano kuanzia Juni 17 hadi 21, 2025.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.