Vijana 30 wilayani Mafia wamepatiwa mafunzo ya uongozaji wa watalii pamoja na sanaa ya ngoma za asili yaliyolenga kuwajengea uwezo katika masuala ya utalii.
Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) kwa kushirikiana na Shirika linalojihusisha na Uhifadhi wa Mazingira na Utunzaji wa Papa Potwe (WATONET), Chuo cha Taifa cha Utalii pamoja na Taasisi ya TACCI yamelenga kuchagiza shughuli za utalii wilayani pamoja na kuwatengenezea ajira vijana.
" Waongoza watalii wana nafasi kubwa sana kwenye kuutangaza utalii, kwa sababu wao wanatoa huduma na kuwapokea wageni. Tukiwa na waongoza watalii ambao hawana weledi na taaluma, taswira ya eneo ambalo watalii wanakuja inakuwa si nzuri" alisema Mtendaji Mkuu wa Shirika la WATONET, Ndugu Juma Salum.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Ndugu Mussa Kitungi, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo hayo, amewataka vijana hao kutumia fursa hiyo kuitangaza Mafia katika utalii na kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukuza sekta ya utalii nchini.
Hii ni awamu ya pili ya utoaji wa mafunzo hayo ambapo kwa mwaka 2023, vijana 25 kutoka kata 6 walishiriki mafunzo ya uongozaji utalii pekee kwa kulinganisha na mwaka huu 2024 ambapo Shirika la WATONET limetanua wigo kwa kuongeza mafunzo ya ngoma za asili ambayo yalitolewa mkoani Morogoro na taasisi ya TACCI.
" Tunaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kwa kutoa kibali cha mafunzo hayo, pamoja na Shirika la WWF na WATONET kwa kushirikiana na wakufunzi wetu kwa kutupa mafunzo haya. Tunaomba kutambuliwa rasmi wilayani kwa kupata vitambulisho ili tuweze kutambulika kisheria na kutunza ajira zetu" alisema Amini Abdallah, kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo ya waongoza watalii.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.