Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Zephania Sumaye ameongoza kikao cha Wadau wa Elimu wilayani Mafia chenye lengo la kujadili kwa pamoja mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya Elimu, changamoto zinazoikabili sekta hiyo pamoja na kutafuta ufumbuzi wa kudumu juu ya changamoto hizo.
Akifungua kikao hicho leo Februari 12, Mhe.Sumaye amewaambia wajumbe na wadau wa kikao hicho kuwa suala la elimu ni miongoni mwa haki za msingi za binadamu na hivyo wanapokaa na kujadili maendeleo ya elimu, wanaimarisha misingi ya haki za binadamu.
Mhe. Sumaye ameongeza kuwa wakati suala la elimu likijadiliwa wilayani Mafia, lionekane kuwa ni jambo litakaloleta mabadiliko si tu kwa Tanzania bali bara zima la Afrika na kusisitiza kuwa misaada yenye kudhalilisha utu wa Watanzania haina nafasi.
Akisoma Taarifa ya Elimu Wilayani Mafia, Afisa Taaluma Elimu Msingi na Awali ndugu Ephata Kaale ameeleza kuwa ufaulu kwa shule za Sekondari kidato cha nne umepanda kutoka asilimia 89.1 mwaka 2022 mpaka asilimia 96.1% wakati kwa upande wa elimu msingi ufaulu kwa darasa la saba kwa mwaka 2023 umeshuka kwa asilimia 8 ikilinganishwa na mwaka 2022.
Pamoja na kujadili suala la ufaulu, wadau wa elimu kwa pamoja walipata nafasi ya kujadili changamoto ya upungufu wa madawati, viti na meza na kuazimia kuchanga kwa hali na mali kuhakikisha changamoto hiyo inakuwa historia.
Aidha wadau wameazimia kuwekwa kwa sheria ndogo juu ya suala la kuchangia chakula shuleni pamoja na Kushauri kuwa jamii ihamasishwe kuchanga fedha kwa ajili ya kugharamikia posho ya walimu wa kujitolea ikiwa ni hatua ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kuajiri walimu wapya.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Mafia amepiga marufuku ufanyikaji wa biashara ya vyakula katika maeneo yote ya shule za msingi na sekondari wilayani Mafia na kuwataka wazazi kuweka jitihada katika kuwapatia watoto wao chakula cha mchana.
Zawadi mbalimbali zimetolewa kwa wadau waliotoa michango yao katika mafanikio ya kitaaluma kwa mwaka 2023 huku shule zilizofanya vizuri kitaaluma nazo zikipatiwa tuzo za vyeti na ngao.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.