Wananchi pamoja na wadau wilayani Mafia wameaswa kushirikiana kwa pamoja kutunza mazingira kwa kutokomeza taka ngumu hasa plastiki ambazo zimekuwa zikiharibu mazingira hasa baharini.
Wito huo umetolewa Oktoba 2, 2025 wakati wa kikao cha kuandaa mpango mkakati na mpango kazi wa pamoja wa kudhibiti taka ngumu hasa za plastiki kwa kuthibitisha taarifa za awali zilizokusanywa na mshauri mwelekezi.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Seleman Kataga ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa mazingira na wananchi kushirikiana kwa karibu zaidi kutekeleza mpango mkakati huo ili kuweza kutokomeza plastiki zinazoendelea kuharibu mazingira.
Kwa upande wake, Afisa Afya wa Wilaya ya Mafia Ndugu Othman Masanga ameeleza kuwa ana imani mpango mkakati unaoandaliwa utasaidia kuboresha shughuli za kiuchumi kama vile utalii ambao unategemea zaidi uhifadhi wa mazingira.


" Kisiwa cha Mafia kinazungukwa na bahari nankinategemea sana shughuli za uvuvi na utalii, hivyo mpango mkakati huu utasaidia kuendeleza bayoanuai za bahari kwa kuthibiti plastiki" alieleza Ndugu Masanga.
Baadhi ya wadau wa mazingira wamepongeza hatua hiyo itakayosaidia uhifadhi wa mazingira kwa kutekeleza maazimio yatakayopendekezwa ili kuzuia ueneaji wa plastiki.
" Kuundwa kwa mfumo jumuishi wa udhibiti taka kwetu ni fursa kubwa kutekeleza kwa pamoja na wadau wengine ili tutokomeze plastiki" alieleza Abdul Amrani, kutoka kikundi cha Takataka Dampo.


Mpango mkakati huo utaenda kutekeleza mradi wa " Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu" unaoratibiwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya FORUMCC kwa kushirikiana na IUCN, Ofisi ya Makamu wa Rais, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia pamoja na wadau mbalimbali wa mazingira na wananchi.
" Natoa wito kwa wadau wa maendeleo, Serikali, asasi zisizo za kiserikali na wananchi kuungana kwa pamoja na kusimamia mpango huu ili uweze kutekelezwa na kuwa endelevu kwa maisha yetu ya baadaye" alisisitiza Gladness Lauwo, Afisa kutoka taasisi ya FORUMCC.


Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.