Wakulima wa mwani wilayani Mafia waaswa kuanzisha ushirika ili kuleta maendeleo katika zao hilo.
Ushauri huo umetolewa leo Aprili 30, 2025 wakati wa kikao cha wadau wa mwani kilichoongozwa na shirika la Action Aid kwa kuhusisha wataalam kutoka Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Divisheni na Vitengo vingine wilayani pamoja na wakulima wa mwani.
"Sisi kama Action Aid, tutaendelea kushirikiana na Serikali, wadau na jamii kwa ujumla kuhakikisha kilimo cha mwani kinapata maendeleo" alisema Samwel Mesiack, Mratibu wa Shirika la Action Aid wilayani Mafia.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wakulima wa mwani kuunda ushirika kukabiliana na changamoto zinazowakabili ili kukuza na kuongeza thamani ya zao la mwani.
Kwa upande wake, Afisa Tawala wilaya ya Mafia Ndugu Jovinus Kyaruzi ametoa wito kwa wakulima kufanya kazi kwa bidii kukuza zao la mwani kwakuwa Serikali ina malengo makubwa katika kuendeleza zao hilo.
"Kama Serikali tutaendelea kutilia mkazo kwa kuchukua hatua stahiki ili kilimo cha mwani kiendelee kuwa na tija, nitoe rai kwa wakulima wote na viongozi wa ushirika kuchapa kazi kwa uzalendo kuboresha maslahi ya wakulima" alisema Ndugu Kyaruzi.
Katika hatua nyingine, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imeweka wazi lengo lake la kuhakikisha wakulima wa zao la mwani wanapiga hatua kwa kutoa ushirikiano wa dhati kutatua changamoto.
" Kama Serikali, kabla ya mwaka kuisha tutafanya sensa ya wakulima wa mwani ili kutusaidia kupanga mikakati ya namna ya kuboresha zao la mwani" alisema Ndugu Mohammed Othman, kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ambaye ametoa wito pia kwa wakulima kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kuendelea kuwekeza kwenye shughuli zao.
Wakulima wa mwani walipata fursa ya kujadili changamoto zinazowakabili na kutoa mapendekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuboresha biashara ya zao hilo kwa lengo la kukuza uchumi wao, Wilaya na Taifa kwa ujumla.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.