Walimu wilayani Mafia waaswa kufanya kazi kwa bidii kwa kutoa huduma nzuri kwa jamii hasa katika kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafaulu vizuri masomo yao.
Wito huo umetolewa leo Machi 27 na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania ( CWT), Mwl. Herbert Ngimi wakati wa zoezi la uchaguzi wa viongozi wa Chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, Chicco.
Mwl. Ngimi amesema kwamba ni muhimu walimu kufanya kazi kwa bidii kwani wao ni kioo na jamii inawategemea.
" Natoa wito kwa walimu na wananchi kwa ujumla kuendelea kukiamini Chama cha Walimu kwani ni sauti ya walimu wote na ni Chama pekee kinachogusa watu wengi" ameeleza .
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mafia na mgeni rasmi katika tukio hilo, Mhe. Aziza Mangosongo amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha elimu nchini kwa kuwajali walimu kimaslahi pamoja na kuongeza watumishi katika sekta hiyo wilayani na kote nchini.
Aidha amewataka walimu kuzingatia maadili na weledi wawapo katika majukumu yao.
Viongozi waliochaguliwa wameahidi kuwa wazalendo kwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa ili kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii.
" Tunaahidi kwamba tunaenda kuwatetea walimu katika wilaya yetu na kuwapambania ili kupata haki zao za msingi katika kuendeleza Chama chetu na wilaya. Natoa wito kwamba tuweze kushirikiana na kusaidiana ili tuwe mfano wa kuigwa kwa vyama vingine vya wafanyakazi na jamii kwa ujumla" alisema Mariam Khalfani, Mwakilishi wa Walimu Wanawake wilaya ya Mafia.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.