Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa ambao hawakuweza kuboresha taarifa zao wakati wa awamu ya kwanza ya zoezi hili, kujitokeza kwa wingi awamu hii ya pili ili wapate uhalali wa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Jaji Mwambegele ametoa wito huo leo Mei 16, 2025 katika kituo cha shule ya msingi Ndagoni alipotembelea kuangalia mwenendo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika kwa siku saba hadi Mei 22, 2025.
" Nimeshuhudia ufunguzi wa zoezi hili katika shule ya Msingi Kilimahewa na kutembelea vituo kadhaa vya jimbo hili, nashukuru zoezi linaendelea vizuri. Ningependa kuwasihi Watanzania kujitokeza kuboresha taarifa zao au kujiandikisha maana usipojitokeza huu mzunguko wa pili, itakuwa ngumu kupiga kura kwahiyo Watanzania wajitokeze kukamilisha haki yao ili waweze kupiga kura" alieleza Jaji Mwambegele.
Aidha, amewataka wananchi ambao ndugu zao wamekosa sifa ya kupiga kura; hasa wananchi ambao ndugu zao wamefariki wajitokeze kwenda kufuta taarifa zao.
Kwa upande wake, Afisa Mwandishikishaji wa Jimbo la Mafia Ndugu Mohamed Othman amewataka wananchi ambao walijiandikisha katika awamu ya kwanza ya zoezi, kuendelea kujitokeza kuhakiki taarifa zao kama zipo sawa bila kusubiri siku za mwisho za zoezi.
Mkoa wa pwani ni miongoni mwa mikoa 16 Tanzania ambayo imeanza zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo mikoa 11 ipo Tanzania Bara na mikoa mitano ipo Zanzibar.
" Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora "
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.