Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, leo Julai 4, 2025 imeongoza mafunzo kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika dirisha la pili kwa mwaka 2024/ 2025.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri yamelenga kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya uendeshaji wa vikundi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo ambazo zitawasaidia katika shughuli zao za ujasiriamali pamoja na kuwawezesha kufanya marejesho.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Maulid Majala amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia wanayojifunza pamoja na kuwa waaminifu katika kufanya marejesho ili mikopo hiyo iwanufaishe wananchi wengi.
Wanufaika wa mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapa fursa hiyo ambayo inawasaidia kuendesha shughuli zao za kila siku na kuahidi kurejesha mikopo hiyo kwa uaminifu.
" Sikuwahi kufikiria kwamba na mimi siku moja nitapata mkopo, naishukuru Serikali kwa kututhamini na naahidi kurejesha mkopo kama inavyotakiwa. Natoa wito kwa vijana wenzangu na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa hii ili wote tujikwamue kiuchumi" alieleza Athumani Rashidi, mkazi wa Kilindoni mwenye ulemavu.
Jumla ya Shilingi Milioni 159 zimetolewa kwa makundi 21 katika dirisha la pili la uombaji wa mkopo wa asilimia 10 ambapo wanufaika wanatarajia kuendelea na mafunzo kwa siku ya kesho Julai 5, 2025.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.