Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo amekitaka kikosi kazi kuhakikisha kuwa kinamaliza tatizo la uvuvi haramu kwa kuimarisha ulinzi baharini ikiwemo kufanya doria na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.
Mhe. Mangosongo ametoa agizo hilo leo Oktoba 17, 2025 wakati wa kikao chake na manahodha, wamiliki wa vyombo, wavuvi pamoja na viongozi wa BMU wilayani Mafia ambapo ameeleza nia ya Serikali katika kukomesha vitendo vya uvuvi haramu ambavyo vimekuwa vikipotosha mapato pamoja na kuharibu rasilimali.
Kwa upande wake, Afisa Uvuvi wa Wilaya Ndugu Alfahad Mohamed ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo, manahodha na wavuvi kuzingatia sheria katika kazi zao ili kuepuka migogoro kati yao na Serikali pamoja na kuhakikisha kuwa wilaya inakuwa na rasilimali endelevu.


Wavuvi pamoja na viongozi wa BMU wameiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwajengea uwezo zaidi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ubora ikiwemo kusaidia katika kutokomeza uvuvi haramu pamoja na masuala ya uhifadhi wa rasilimali zilizopo kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo yao.
"Tunashukuru kwa nafasi hii kukutana na kujadili, sisi changamoto tunayoipata katika shughuli yetu ni uvuvi haramu ambao mara nyingi unafanyika usiku, hivyo tunaomba tuimarishiwe ulinzi kwa kupatiwa vifaa ikiwemo kamera za kutusaidia kuwafuatilia pamoja na machine kwa ajili ya boti yetu ya doria" alieleza Bakari Mgaza, Mwenyekiti wa BMU kijiji cha Jojo.
Katika hatua nyingine ya kukomesha vitendo viovu wilayani Mafia, Mhe. Mangosongo ametoa wito kwa wavuvi kwa nafasi zao kuhakikisha kuwa wanakuwa mstari wa mbele katika kukemea vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, ulevi uliokithiri pamoja na zinaa huku akitilia mkazo kutokujihusisha na wanawake wanaojiuza maarufu kama ' vijoti ' ambao wameenea kwa wingi katika maeneo mbalimbali.


Mhe. Mangosongo ameeleza kuwa ni muhimu kuzingatia sheria ndogo zilizopo wilayani ikiwemo zinazohusu mavazi katika jamii pamoja na kuwataka wamiliki wa sehemu za starehe kuzingatia sheria kama vile kufanya biashara zilizolengwa kutokana na vibali vyao bila kuruhusu biashara zisizofaa ambazo zimekuwa zikichangia kuleta mambo ambayo ni kinyume na maadili.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.