Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mbunge wa Mafia Mhe. Omar Kipanga ametoa rai kwa wadau wote wa elimu wakiwemo viongozi na walimu kutoa ushirikiano kwa Serikali na wataalam mbalimbali ili kuhakikisha jamii inahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi.
Mhe. Kipanga ametoa rai hiyo leo Mei 17, 2025 wakati wa ufunguzi wa mradi wa uhamasishaji wa wanafunzi wa kike kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu ( STEM) utakaotekelezwa na Tume ya Taifa ya UNESCO (Natcom) kwa kufadhiliwa na UNESCO.
" Mradi huu umekuja wakati mwafaka, wote tunazifahamu na kuendelea kuzifuatilia jitihada zinazofanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita, hivyo naomba tutoe ushirikiano kwa wataalam wetu kuhakikisha jamii inahamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya STEM" alisema Mhe. Kipanga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Sayansi Asilia kutoka Tume ya Taifa ya UNESCO Dkt. Joel Samuel ambaye amemuwakilisha Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, amesema kuwa Tume kupitia mradi huu itafanyia kazi pia changamoto ya walimu wa sayansi ili kuhakikisha mradi huu unakuwa endelevu na kusaidia wanafunzi wa kike kupenda na kufanya vizuri katika masomo ya Sayansi , Teknolojia, Uhandisi na Hesabu.
Baadhi ya wazazi walioshiriki ufunguzi wa mradi huo wameahidi kushirikiana na walimu kuwahamasisha watoto wa kike wapende masomo ya sayansi ambayo mara nyingi wamekuwa wakiyaogopa
" Mimi nitakuwa balozi kwa kupita kila shule katika kata yangu kuongea na wanafunzi ili waweze kuyapenda masomo ya sayansi , pia nitahamasisha wazazi wenzangu kuwatia moyo watoto wa kike wapende masomo ya sayansi" ameeleza Mwajuma Ibrahim, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi kata ya Kiegeani na mjumbe wa bodi ya shule ya sekondari Kitomondo.
Idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mchepuo wa sayansi kwa sekondari imeongezeka kutoka 21 mwaka 2020 hadi kufika 55 mwaka 2023, hata hivyo, wanafunzi wa kike wanaojiunga na mchepuo wa sayansi ni wachache kulinganisha na idadi ya wanafunzi wa kiume ambapo ufaulu pia ni mzuri kwa wanafunzi wa kiume kuliko wa kike.
" Natamani tuendelee kupiga kampeni kuhakikisha watoto wa kike wanafikia ndoto zao bila kukatishwa kwa sababu kadhaa ikiwemo ujauzito, tukiwasimamia vizuri tutafanikiwa kupata wanafunzi wa kike wa masomo ya sayansi" alisema Bi. Khadija Mohamed, mwalimu wa somo la Baiolojia kutoka shule ya sekondari Kitomondo.
" Walimu ni watu wa kwanza wa kufanya watoto wa kike wapende masomo ya sayansi, hivyo tutengeneze urafiki kwa watoto wetu wa kike ili wapende masomo ya sayansi". Kwa upande wangu, mwaka 2024 kwa kidato cha nne, wanafunzi 100 walifaulu somo la Baiolojia na kulikuwa na alama 'A' moja ambayo aliipata mtoto wa kike, na alama B za kutosha pamoja na alama C . Alieleza.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozaji wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada nyingi kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora, miongoni mwa Juhudi hizo ni pamoja na ujenzi wa shule maalum 26 za sayansi za wasichana katika mikoa, ujenzi wa bweni kwa wanafunzi wa kike kuwapunguzia umbali waendapo shule, utungaji na utekelezaji wa sheria na miongozo mbalimbali inayotoa fursa kwa wanafunzi wa kike kutimiza ndoto zao, wanafunzi wanawake kupewa kipaumbele katika programu mbalimbali kama vile ufadhili wa masomo " Samia Scholarship" na kuimarisha mifumo ya utawala bora.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.