Miradi ya maji inayosimamiwa na kutekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA), inatarajiwa kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji Safi na Salama wilayani Mafia kwa kumtua mama ndoo kichwani.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi inayoendelea kutekelezwa na RUWASA katika baadhi ya maeneo zikiwemo kata za Kilindoni na Kiegeani.
Ili kufanikisha hayo, Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Billioni saba kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa Maji Safi na Salama kwa wananchi wa wilaya ya Mafia.
" Lengo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumtua mama ndoo kichwani haliwezi kutimia kama miradi hii haitasambazwa na kufikia wananchi kote" alisema Mhe. Mangosongo.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA wilaya ya Mafia Mhandisi Clement Lyoto ameahidi kukamilisha kwa wakati miradi yote wanayosimamia pamoja na kuiomba jamii kushirikiana katika kuilinda na kuitunza Miradi hiyo.
Mhe. Mangosongo amewataka wasimamizi wa miradi kushirikisha wananchi kikamilifu katika kutekeleza miradi hiyo, ambapo amewapongeza na kuwashukuru wananchi wanaojitolea maeneo yao ili kuhakikisha jamii inanufaika.
Baadhi ya wananchi waliopata bahati ya kuhudhiria kwenye miradi hiyo wameishukuru serikali kwa kuwafikishia huduma hizo kwa karibu pamoja na kuahidi kuitunza pindi itakapo kamilika ili iweze kuwanufaisha wao na vizazi vijavyo.
" Mradi huu sisi wananchi tunautaka sana, mradi utapokamilika, maisha yetu yatakuwa mazuri sana hasa kwa sisi tunaofanya shughuli za kilimo" alisema Ahmad Bakari, mkazi wa kitongoji cha Kitundu, kijiji cha Dongo ambapo mradi wa maji wa kisima unatekelezwa.
Miradi inayotekelezwa na RUWASA wilayani Mafia ni pamoja na ujenzi wa matenki makubwa ya maji, visima na ofisi za maji.
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.