Posted on: March 22nd, 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (Mb) amefanya ziara ya kukagua miundombinu ya barabara katika halmashauri ya wilaya ya mafia . Akiwa ziarani Mhe. Waziri ameagiza Wakala wa Barabara
( TANROADS) kuhakikisha barabara ya Kilindoni-Rasi Mkumbi yenye urefu wa zaidi ya Kilomita 50 inakamilika kwa kiwango cha changarawe kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na taratibu za kumpata mkandarasi ili kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Bashungwa ametoa maagizo hayo Machi 22 wilayani Mafia wakati wa ziara yake ya kukagua miundombinu ya barabara ikiwemo barabara ya Kilindoni-Utende ( KM 14.6) yenye kiwango cha lami na barabara ya Kilindoni-Rasi Mkumbi (KM 54.4) ambapo Kilomita 2.2 kati ya hizo zimekamilika kwa kiwango cha lami.
" Kwa dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifungua Mafia, inabidi tuhakikishe kuna mawasiliano mazuri ya barabara. Wakati huu tukiendelea na taratibu za kumpata Mkandarasi kumalizia kipande kilichobaki, TANROADS ihakikishe barabara hii inakamilika kwa kiwango cha changarawe ili iweze kutumika vizuri" alisema Bashungwa.
Aidha, amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kutowapatia kazi wahandisi washauri ambao wanaisababishia hasara Serikali kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kusimamia vizuri miradi.
Sambamba na ukaguzi wa miundombinu ya barabara, Waziri Bashungwa alipata nafasi ya kutembelea na kukagua kivuko cha Kilindoni ambapo alikutana na kuzungumza na wafanyakazi pamoja na wafanyabiashara ambao husafirisha mizigo yao kupitia kivuko hicho ili kuweza kujua changamoto wanazokutana nazo.
"Tuna changamoto ambazo tunazipata kutokana na mazingira ya bandari yetu, hatuna sehemu za kuhifadhia mizigo wala vitendea kazi, hivyo kusababisha hasara kwenye mali zetu. Tunaomba Serikali itusikilize na kutusaidia" alisema Mohammed, mfanyabiashara wa Mafia.
Kufuatia kero hizo, Waziri Bashungwa alitoa maagizo kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuhakikisha wanafanya maboresho ya huduma za vivuko wilayani Mafia na kote nchini kwa ajili ya usalama wa abiria na mali zao
Kilindoni-Bomani Street
Anuani ya posta: 85
Simu: 0232010199
Simu ya mkononi:
Baruapepe: ded.mafia@pwani.go.tz / ded@mafiadc.go.tz
Copyright ©2017 Mafia District Council . All rights reserved.